Mahakama ya hakimu mkazi Kinondoni jijini Dar es salaam imesitisha
kwa muda shughuli zake baada ya zomeazomea iliyosababishwa na umati
mkubwa wa watu waliofika mahakamani hapo kushuhudia kesi inayomkabili
Amina Maige aliyeshitakiwa kwa kosa la kumjeruhi binti kwa kumng'ata na
kumuunguza kwa pasi.
Wakili Mohamed amesema upelelezi umekamilika ambapo
mshitakiwa amekana shitaka hilo na kurudishwa rumande baada ya
mwendesha mashitaka huyo kumuomba hakimu asimpatie dhamana kwa ajili ya
usalama wake, ombi ambalo hakimu alikubaliana nalo ambapo mtuhumiwa
amerudishwa rumande hadi June 26 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa kwa
ajili ya masikilizo ya awali.
Ndivyo hali ilivyokuwa katika mahakama hiyo mara
baada ya mtuhumiwa huyo kufikishwa mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi
mkali wa polisi ambapo kabla ya kuteremka kutoka ndani ya gari
alifunika uso wake na mtandio hali iliyosababisha umati huo kuanza
kupiga kelele wakitaka afunuliwe ili aonekane.
Hata mara baada ya kuhifadhiwa katika chumba cha
maabusu ya mahakama hiyo wakati akisubiri kupandishwa kizimbani baadhi
ya wanaharakati waliofika mahakamani hapo nao walisikika wakilaani
kitendo cha polisi kumsaidia kufunika uso kama wanavyosikika.
Zoezi la kuwatuliza wananchi hao lilionekana
kuwashinda askari wa jeshi la polisi hali iliyowalazimu askari magereza
kuingilia kati na kusaidiana nao ili shughuli za mahakama ziweze
kuendelea kama askari huyu alivyosikika akiwaomba waondoke katika eneo
hilo.
Akisoma shitaka linalomkabili mtuhumiwa huyo wakili
wa serikali Mohamed Salum mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya
Kinondoni Yohana Yongolo amesema mtuhumiwa amina maige anakabiliwa na
kosa la kumjeruhi vibaya Binti Eusta Hashim kinyume na kifungu kidogo
cha sheria 225, kosa alililolitenda huko eneo la Mwananyamala Manjunju.