WASOMALI 1541 WAPEWA URAIA NCHINI

SERIKALI ya Tanzania imetoa uraia kwa wakimbizi 1,541 wa Somalia waliokuwa wanaishi katika Makazi ya Chogo, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Watu hao waliikimbia Somalia mwaka 1990 baada ya kuibuka kwavita nchini mwao ambapo 3,000 kati yao walikimbia Tanzania walikopokelewa na kuhifadhiwa katika Kambi ya Mkuyu iliyopo mkoani Tanga ambapo walikuwa wakipata msaada kutoka Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja waMataifa (UNHCR).

Akizungumza jana baada ya kuwapavyeti vya uraia wakimbizi hao ambao kwasasa ni raia halali wa Tanzania, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema wakimbizi hao walihamishwa na Serikali mwaka 2003 kutoka Kambi ya Mkuyu kuja katika makazi ya Chogo ili wapatiwe mashamba kwa ajili ya kujishughulisha na kilimo ili waweze kujitegemea.

"Nachukua nafasi hii kuwapongeza wote waliopewa uraia wa Tanzania, wajisikie kuwa wao ni raia huru sawa na Watanzania wengine. Hata hivyo nawasihi muwe waadilifu na watiifu kwa sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," alisema Chikawe.

Chikawe pia alitoa pongezi kwa UNHCR kwa kujenga miundombinu muhimu katika makazi hayo ya Chogo na pia kuwawezesha wakimbizi hao kuishi maisha ya kujitegemea kabla hata ya kuwa raia.

Hata hivyo, Waziri Chikawe aliwataka wakimbizi 150 katika makazi hayo ya Chogo ambao hawakuomba kuwa raia wa Tanzania kwa nia ya kurudi nchini Somalia pale hali ya amani itakapopatikana wanapaswa kuendelea kutii sheria za nchi zinazotawala hifadhi ya ukimbizi nchini.

Aidha, Mwakilishi Mkazi wa UNHCR, Joyce Mends-Cole katika hafla hiyo aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapa uraia wakimbizi hao na Shirika lake litaendelea kutoa misaada mbalimbali kwa wakimbizi waliobaki katika makazi hayo pamoja na sehemu nyingine nchini.

Hafla hiyo ya ugawaji wa vyeti vya uraia ilihudhuriwa na maofisa wa Idara ya Wakimbizi na Uhamiaji zilizopo Wizara ya Mambo ya Ndaniya Nchi, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Serikali ya Kijiji cha Chogo na maofisa wa UNHCR.