KATIBU MKUU AMTISHIA KAFULILA

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi ameibuka na kuzungumzia sakata la kuitwa Mwizi na Mbunge wa Kigoma Kusini,David Kafulila (NCCR –Mageuzi )na kumtaka kama ana ubavu azungumzie nje ya Bunge.


Akizungumza na Waandishi wa habari jana kuhusu Serikali kupitisha Mkakati na Mwelekeo wa Sekta Ndogo ya Umeme (ESI), alisema wabunge wamekuwa wakizungumzia masuala hayo ya kashfa bungeni kutokana na kuwa na kinga.

"Kama ana uhakika wa jambo hilo kuwa mimi ni mwizi aje aseme hadharani kama ilivyo hapa na siyo ndani ya Bunge, aone kama sijamfikisha mahakamani, kwani akiwa ndani ya Bunge anajifanya mwanaume kweli kumbe m***'," alisema.


Alisema kuwa kuna unafiki umejaa na unaenezwa kwa vipeperushi na kushabikiwa na baadhi ya waandishi wa habari wakidai kuwa anahusika na ufisadi wa zaidi ya Sh bilioni 200 katika akaunti ya Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).


Maswi alisema yeye binafsi anajiamini hachukui rushwa hivyo anaruhusu yeyote anayetaka kupata uhakika amfuatilie na yeye atawaonyesha jinsi alivyopata mali zake zote .

"Njooni nitawaonesha nilivyopata mali zote nilizonazo na yeye Kafulila kama mwanaume kweli aseme nje ya bunge kwani atanitambua nitakavyo mshughulikia, t***i kweli yule,"alisema.


Alipoulizwa anadhani ni kwa nini Kafulila amekuwa na nguvu za kumtaja hadharani kama anahusika na tuhuma hizo, Maswi alimtaka Kafulila na wabunge wengine kutotumia bunge kusema uongo kwa kuwa wana kinga bali watoe ushahidi wa wizi wanaoujua.


Maswi alisema pia anamjua Kafulila na hawezi kusimama na kusema hadharani anayotamba bungeni kwani kutokana na kuwa sio mwanasiasa na amelelewa na anajua maadili.


"Kama hakulelewa vizuri, atalelewa na dunia kama wahenga walivyosema kwani nina usongo naye sana kwa kuwa najua ana makaratasi ya kufungia vitumbua na kudai ni ushahidi jambo ambalo serikali haitishiwi,"

alisema Maswi alikuwa akijibu hoja za Kafulila, baada ya kuulizwa na waandishi wa habari ni jinsi gani watakabiliana na matumizi mabaya ya fedha katika wizara hiyo wakati wa uboreshaji wa sekta ya umeme.