MTOTO WA MIAKA 18 HAJALIA TANGU AZALIWE

TUKIO la mtoto Nasra Mvungi kuteswa kwa kufungiwa katika boksi ndani ya nyumba kwa zaidi ya miaka mitatu na kufariki dunia baada ya kuokolewa na wasamaria, limefanikisha kupatikana kwa mtoto mwingine mwenye matatizoya kiafya ambaye licha ya kuzaliwa miaka 18 iliyopita, inaelezwa hajawahi kulia, kuongea, kukaa wala kutembea.

Mtoto huyo mwenye mwonekano kama wa mtoto mwenye umri wa miaka mitano, amepatikana baada ya wasamaria kutoa taarifa Dawati la Jinsia katika Jeshi la Polisi wilayani hapa, wakiarifu kuwapo kwa mtoto mlemavu anayenyanyaswa kama ilivyokuwa kwa mtoto Nasra `Mtoto wa Boksi'.

Katibu wa Dawati la Jinsia, Koplo Janeth Maeda amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo, akisema walipokea taarifa za kuwapo kwa mtoto anayenyanyaswa, hivyo kukimbilia eneo la tukio ili kumwokoa mtoto aliyedaiwa kuwapo katika mateso ikiwa pamoja na kunyimwa huduma muhimu.

Hata hivyo, anasema walichokishuhudia si mateso, bali ni hali duni ya kimaisha ya wazazi wake, hivyo kulilazimu Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ustawi wa Jamii kumwokoa kwa kumkimbiza hospitali kwa uchunguzi zaidi wa afya yake.

Anasema: "Kwa kweli tulipopata taarifa hizo tulishtuka sana tukaamua kuwasha gari na kuelekea eneo la Lukobe ambako ndiko tuliambiwa kuwa kuna mtotohuyo na kumkuta mtoto huyo, lakini tofauti na tulivyoambiwa, tulimkuta akiwa katika mazingira mazuri."

"Labda kilichoonekana kwa wengine kama ni mateso ni kwa sababu wazazi wake kutokuwa na uwezo wa kumudu matibabu tumeamua kusaidiana na ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa kumsaidia mtoto huyo kwa kuhakikisha anapatiwa huduma ya matibabu anayostahili."

Kwa mujibu wa wazazi wa mtoto huyo wa kike aitwaye Farida, baba Abdallah Kipingu na mkewe, Mwajuma Abdallah, wakazi wa Lukobe katika Manispaa ya Morogoro, binti yao huyo alizaliwa mwaka 1996 na kwamba tangu azaliwe hajawahi kulia.

Mama wa mtoto, Mwajuma akiwa sambamba na mumewe alisema walimzaa Farida huko Muheza mkoani Tanga na kwamba walimzalia nyumbani, lakini kutokana na kushindwa kulia, wiki moja baadaye walikwenda Hospitali ya Wilaya ya Muheza ili kujua kilichomsibu mtoto wao."

Hatukupata msaada, tukaendelea kumlea alipofikisha miezi minne ambao mara nyingi ni muda wa kukaa, tulijaribisha kumkalisha, lakini hakukaa hivyo kwa mara nyingine tukaenda hospitali, safari hii ya Mkoa wa Morogoro ambako tumekuwa tunaishi, tukaambiwa mtoto ahudhurie mazoezi ya viungo.

"Tulihudhuria mazoezi kwa muda mrefu hatukuona mabadiliko baadaye tukaamua kuhamia kwenye kituo cha kulea watoto walemavu cha Amani Center, tukaambiwa tuendelee ingawa hakukuwa na mabadiliko, tulipohamia Lukobe mwaka jana hatukuweza tena kumpeleka kwenye mazoezi kutokana na kukosa uwezo wa kifedha za kufanya mizunguko," anasema.

Anasema wamekuwa wakiendesha maisha kwa kutegemea biashara yabidhaa ndogondogo katika genge lao, msimamizi mkuu akiwa mumewe na kwamba yeye huhangaika zaidi na mtoto.

"Hayo ndiyo yamekuwa maisha yetu hadi kufikia wakati huu tulipopata msaada wa Polisi na Ustawi wa Jamii," anasema mama huyo aliyeiomba jamii kuwaombea na kuwapa msaada wa hali na mali katika kufanikisha matibabu na malezi ya binti yao ambaye kwa sasa amefikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa uchunguzi zaidi.

Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu aliwashukuru wananchi kwa kuitikia mwito wa kutoa taarifa za matukio kama ya mtoto Nasra, kwani imewafanya wafumbue macho na kutoa taarifa mbalimbali.

Alisema taarifa zao zinaweza kuwa faraja kwa watoto na wazazi wengi wasiojua cha kufanya baada ya kuelemewa na majukumu ya kutunza watoto wenye uhitaji maalumu.

Hata hivyo, aliitaka jamii kuwapeleka watoto wenye ulemavu na wenye matatizo katika sehemu zinazohusika ili watoto hao waweze kupatiwa msaada na hatimaye kuweza kuimarisha afya zao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mganga Mkuu Mfawidhi, Dk Rita Lyamuya alisema baada ya kupata taarifa hizo taratibu za kumfanyia uchunguzi zinaendelea ikiwa ni pamoja na kumpatia virutubisho.