Mtuhumiwa huyo ni Hamisi Othman Mzee maarufu kwa jina la Hamisi Mabunduki(44), Mkazi wa Zanzibar na Dar es Salaam.
Akithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Yusuf Msige alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa katika kijiji cha Matale wilaya ya Chakechake akiwa mafichoni.
Kamanda Msige alisema Polisi inawasiliana na wenzao wa Mkoa wa Pwani kwa upelelezi zaidi.
Katika uvamizi wa kituo na mauaji, majambazi hayo yaliwaua Koplo Joseph Ngonyani na Mgambo Venance Mushi aliyekuwa akisaidia ulinzi kituoni hapo kabla ya kupora silaha zaidi.
Kamanda Msige alisema taarifa za kiintelijensia zinaonesha kuwa mtuhumiwa huyo ambaye ni hatari amekuwa akikabiliwa na kesi lukuki za matukio ya ujambazi wa kutumia silaha na alitoka rumande Mei 28 mwaka huu.
Tangu wakati huo mtuhumiwa huyo na genge lake amekuwa akiendeleza matukio ya kihalifu yakiwemo ya uporaji na mauaji katika mikoa mbalimbali.
Kamanda Msige alisema polisi wanaendelea na upelelezi ikiwa ni pamoja na kupata taarifa muhimu za watuhumiwa wengine wanaojificha ili watiwe mbaroni kukabili mkono wa dola.