MAASKOFU WAIKOSOA SERIKALI YA ERITREA

Maaskofu wanne wa kanisa katoliki nchini Eritrea, wamechapisha barua inayokosoa mfumo wa maisha nchini humo, hatua ambayo inaonekana kama yakishujaa ndani ya nchi ambayo uhuru wa kujieleza umebanwa mno.


Ingawa maaskofu hao walijizuia na kulaani au kukosoa serikali, hatua yao pekee ya kuandika barua hiyo inasemekana kuwa hatua kubwa na ambayo wengi wanaitazama kama ya kujiingiza motoni.

Makasisi wamezungumzia idadi kubwa ya raia wa Eritrea waliofariki kisiwani Lampedusa mwaka jana wakisema kuwa hakuna haja ya mhamiaji kutafuta nchi yenye asali wakati nchi yake mwenyewe ni asali tosha.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu, yameitaja Eritrea kama gereza moja kubwa sana ambayo huwatesa wafungwa.


Shirika la Amnesty International mwaka jana lilisema kuwa takriban watu 10,000 walifungwa jela kwa sababu za kisiasa tangu nchi hiyo kujitawala baada ya kupata uhuru kutoka kwa Ethiopia mwaka1993.

Madai haya yamekanushwa na serikali.

Vijana wa Eritrea lazima wajihusishe na shughuli za ujenzi wa taifa hadi wanapofika umri wa miaka 40 hali ambayo imesababisha takriban watu 3,000 kuitoroka nchi hiyo kila mwezi.


Katika barua yao, maaskofu hao waliandika kuwa watu wengi wanaitoroka nchi hiyo kwa hivyo watu wakongwe wa taifa kukosa watu wa kuwalea uzeeni.

Walisema kuwa wananchi wa Eritrea wanaelekea katika nchi salama, nchi ambazo zinawapa fursa ya kufanya kazi na ambako wana uhuru wa kujieleza pia nchi ambazo mtu anafanya kazi na kupata malipo.


Barua hiyo ilitiwa saini na maaskofu , Mengsteab Tesfamariam wa Asmara, Tomas Osman wa Barentu, Kidane Yeabio wa Keren na Feqremariam Hagos wa Segeneiti.

Makasisi hao wameitaka serikali kutowatesa wafungwa na pia kuwa na huruma na kisha kuwaruhusu kuwakilishwa mahakamani.


Baada ya kanisa la Orthodox, kanisa la kikatoliki ndilo la pili kwa ukubwa nchini Eritrea na wadadisi wanasema kwamba askofu mkuu wa Asmara,ana ushawishi mkubwa sana nchini humo.