WANAFUNZI WAOA WAKE 3 NA KUACHA MASOMO

HALI si shwari katika sekta ya elimu katika wilaya za Kalambo na Sumbawanga mkoani Rukwa, baadaya kuelezwa idadi kubwa ya wanafunzi wa kiume katika shule za sekondari hukatisha masomo ili kujikita katika kutunza familia, kwani wengi wao ni waume za watu, wengine wakiwa na wake hadi watatu.

Kwa kiasi kikubwa, dhana iliyopo nikwamba wanawake ndio wanaokatishwa masomo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupata ujauzito au kulazimishwa kuolewa katika umri mdogo.

Hayo yalibainika katika kikao cha siku moja cha Wadau wa Elimu kilichowakutanisha Waratibu Elimu Kata, Maofisa Elimu wa Wilaya za Kalambo na Sumbawanga na kufanyika juzi mjini hapa nchini ya uratibu wa Asasi isiyo ya Kiserikali ya TMEP kupitia mradi wake wa afya ya uzazi na ujinsia unaotekelezwa mkoani Rukwa na taasisi isiyo ya Kiserikali ya Resource Oriented Development Initiative (RODI).

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kasanga iliyopo katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Kalambo, Christopher Sinyangwe ndiye aliyeibua hoja, baada ya kueleza kuwa utoro sugu ni changamoto kubwa katika shule hiyo, akisema kati ya wanafunzi 80 wanaoanza kidato cha kwanza, mara nyingi wanaohitimu hawazidi 30.

Aliongeza kuwa sababu kubwa ni mwamko mdogo wa elimu kwa upande wa wazazi na walezi ambao wanawaozesha watoto wao mara tu wanapoingia Kidato cha Kwanza na kuwaacha wake zao katika vijiji wanavyotoka hivyo wanalazimika mara kwa mara kukatiza masomo yao ili waweze kurudi nyumbani kuwajibika kwa familia zao.

"Zipo taarifa za uhakika kuwa wanafunzi wa kiume kuwa na wake wawili hadi watatu…baadhi yao wanaanza Kidato cha Kwanza tayari wameshaoa, wakifika Kidato cha Tatu tayari ana wake watatu au wawili na watoto ambao anawajibika kuwa hudumia hivyo wanakatiza masomo na kujihusishana shughuli za uvuvi kwa muda ili kuzikimu familia zao kisha hurejea shuleni," aliongeza Sinyangwe.

Kwa mujibu wa Kaimu Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Japhet Buchwa ambaye pia ni Ofisa Elimu Taaluma (Sekondari) alibainisha kuwa utoro sugu ni changamoto kubwa shuleni kwa upande shule za umma watoto600 walikatiza masomo yao kwa kipindi cha Januari hadi Februari mwaka huu.

Alisema katika kipindi hicho cha kati ya Januari na Februari mwaka huu wanafunzi wapatao 23 kutoka shule za sekondari za binafsi wamekatiza masomo yao kwa sababu mbalimbali zikiwemo za ujauzito.Kwa mujibu wa Buchwa, watoto wapatao 4,913 wanasoma katika shule za sekondari za umma wilayani humo ambapo shule za sekondari za binafsi zina wanafunzi wapatao 300.

Akichangia uzoefu wake, Mratibu Elimu Kata ya Mfinga katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga alibainisha kuwa kutokana na mwamko duni wa elimu wazazi huwaozesha watoto wao wa kike kwa mahari kati ya ng'ombe 25 hadi 30 pia kwa watotowa kiume wanarubuniwa na wazazi wao kukatiza masomo yao na kuwaajiriwa kama vibarua mashambani na kuchunga mifugo.

"Wengi wa wazazi na walezi ambao hawaoni umuhimu wa elimu wanadai ni bora watoto wao wakaoe au kuolewa kuliko kuendelea na masomo … isitoshe baadhi ya wazazi huwatishia maisha walimu wanapofuatilia watoro sugu," alibainisha.

Naye Mratibu Elimu Kata ya Mpui wilayani Sumbawanga, Tabia Mkembo alibainisha kuwa kutokana na Shule ya Sekondari Mpui kutokuwa na uzio, wanafunzi wa kike wanadaiwa kutoroka usiku na kwenda kufanya ufuska hivyo baadhi yao kupata ujauzito maarufu kama 'mimba za minadani".

Alidai vibarua wa kampuni ya ujenzi inayojenga barabara ya Laela – Sumbawanga kwa kiwango cha lami ni miongoni mwa watuhumiwa wa 'kuoa' watoto wa kike shuleni hapo ambapo baadhi ya wasichana wanaoishi katika hosteli shuleni hapo wanashawishika kutoroka usiku na kwenda kwa 'waume' zao hao kutokana na shule hiyo kutokuwa na uzio.

"Tuna taarifa kuwepo kwa visa kwa wasichana wanaoishi katika mabweni shuleni hapo kutoroka nakwenda kulala katika bweni la wavulana … Hapa walezi wa watotohawa 'patroni ' na 'matroni' wanapaswa kuwafuatilia kwa karibuwatoto hawa," alisisitiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa RODI, Gideon Mpina alizitaka Halmashauri kuunda sheria ndogo ndogo zitakazo zipa nguvu za kisheria mamlaka husika kuwasaka wazazi na walezi wote watakaobainika kuwaozesha watotowao wanaosoma ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.