ISRAEL YAONYWA KUHUSU KUWATAFUTA VIJANA WA 3 WALIOTEKWA

Umoja wa Mataifa umeishauri Israel ijizuie wakati inapowatafuta vijana 3 raia wa nchi hiyo waliotoweka tangu Juni 12 Ukingo wa Magharibi. Afisa wa umoja huo ameonya juu ya kutokea mapinduzi mapya dhidi ya Israel.
Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya siasa, Jeffrey Feltman, amelionya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba msako unaofanywa na Israel katika maeneo ya Wapalestina yumkini ukazusha machafuko zaidi katika eneo hilo. Feltman amesema, na hapa namnukuu, "Wakati Israel ikiwatafuta vijana hawa tunahimiza ijizuie katika kufanya operesheni zake za usalama kwa kufuata sheria za kimataifa," mwisho wa kumnukuu.
Akilihutubia baraza la usalama Jumatatu (23.06.2014) wakati wa mkutano wa kila mwezi kuhusu Mashariki ya Kati, Feltman amesema, "Ongezeko la vifo kutokana na operesheni ya usalama ya Israel katika eneo la Ukingo wa Magharibi linatisha. Tunalaani mauaji ya raia na tunataka kufanyike uchunguzi. Tunaitaka Israel ijiepushe kuwaadhibu watu kwa makosa ambayo kibinafsi hawajayafanya."
Feltman pia amesema hali ni mbaya mno na anahofia huenda kukazuka mapinduzi ya tatu ya intifada dhidi ya Israel.
Bildergalerie Israel Konflikte Wazazi wa mmoja wa vijana wanaotafutwa, Gil-Ad
Hatua ya Israel kuwaadhibu Wapalestina wakati wa zoezi la kuwatafuta vijana hao katika Ukanda wa Gaza imezua ghadhabu miongoni mwa Wapalestina, ambao wameonya tukio hilo linatumiwa kwa masilahi ya kisiasa.

Operesheni yaibua wasiwasi
Hani al-Masri, mwandishi wa habari wa Kipalestina na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, anasema, "Kuendelea kuratibu operesheni ya usalama kati ya Wapalestina na Waisraeli katika mazingira haya kunaifanya mamlaka ya ndani ya Wapalestina kuwa mshirika na dola inayoyakalia maeneo yake. Na ni mbaya sana kwa uaminifu na uhalali wa mamlala hiyo.
Mzozo huo umeibua hali ya wasiwasi katika Ukingo wa Magharibi, ambao pamoja na Jerusalem Mashariki na Ukanda wa Gaza, Wapalestina wanataka liwe taifa lao la siku za usoni. Msemaji wa kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza, Mushir al Masri, ameonya dhidi ya msako wa Israel kutumika kusababisha uhasama kati ya kundi hilo na chama cha Fatah.
"Tunachotakiwa kufanya sasa ni kuendelea mbele na mchakato wa maridhiano kati ya pande hizi mbili bila kujali ushawishi mbaya kutoka kwa Israel. Tuna matumaini Fatah na Hamas hawatazuiwa na Israel na hawatoacha kabisa mchakato huo wa maridhiano."
Israelische Militäraktion im Westjordanland Wapalestina mjini Nablus na maiti ya kijana aliyeuwawa na Israel katika operesheni
Jeshi la Israel limesema limewatia mbaroni Wapalestina wengine 37 usiku wa kuamkia leo huku ikiwatafuta vijana hao na kutanua harakati yake dhidi ya kundi la Hamas, ambalo limeknusha kuwa na taarifa kuwahusu vijana hao wasiojulikana waliko. Jeshi la Israel aidha limesema linawazuia watu 361 tangu wanafunzi hao walipotoweka Juni 12, na limetuma vikosi zaidi vya wanajeshi kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi tangu Juni 13 kuwatafuta vijana hao watatu wa Kiisraeli waliotoweka karibu na mji wa Hebron.