SUPER EAGLES WAGOMEA MAZOEZI

Kikosi cha Nigeria katika kombe la dunia kimesusia kikao cha mazoezi kama ilivyopangwa kwa sababu ya kukosa kulipwa fedha zao za ziada.


Kitengo cha michezo cha BBC kimeelezwa kuwa wachezaji hao wanaamini kuwa wamelipwa kiasi cha dola 15,000 (pauni 8,800), chini ya pesa wanazopaswa kulipwa baada ya kufika katika mkondo wa pili wa kombe la dunia, huko Brazil.


Wachezaji hao wamesusia mazoezi katika uwanja wa Campinas na baadaye maafisa wakadai kwamba mazoezi hayo yalikuwa yametupiliwa mbali.

Nigeria inachuana na Ufaransa katika mechi ya muondowano siku ya Jumatatu baada ya kuchukua nafasi ya pili katika kundi lao la F.


Shirika la habari la BBC michezo limeelezwa kuwa shida imetokea katika ufafanuzi wa njia itakayotumika kuwalipa wachezaji hao pesa hizo za ziada.


Wachezaji hao wanaamini kuwa watapokea dola 10,000 kwa ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Bosnia-Hercegovina na dola 5,000 kwa sare yao dhidi ya Iran.


Wachezaji hao pia wanadhania kuwa wanapaswa kulipwa dola 30,000 kwa kufuzu katika kundi hiyo.


Hata hivyo, inaaminika kuwa ahadi hiyo ya shirikisho la soka la Nigeria kwa wachezaji wake ilijumuisha malipo ya ushindi na kutoka sare na pia asilimia 30 ya pesa watakazolipwa na Fifa kwa kufika katika raundi ya muondowano.


Inaaminika kuwa kitita hicho kinatarajiwa kupanda hadi asilimia 40 kama fedha watakazolipwa na Fifa ikiwa Nigeria watashinda mchuano wao wa raundi ya muondowano, aslimia 50 kwa ushindi wa robo fainali, asilimia 60 kwa ushindi katika nusu fainali na asilimia 70 kwa kushinda kombe hilo la dunia.


Huku Wahusika wote wakifanya juhudi za kupata suluhu ya mtafaruko huo , mkufunzi, Stephen Keshi anasisitiza kuwa swala hilo halitakuwa na madhara yoyote katika timu hiyo.


BBC pia imethibitishiwa kuwa wachezaji hao watasafiri kwenda Brasilia siku ya Ijumaa kama ilivyoratibiwa na kufanya mazoezi yao jioni itakayofuata.

Si mara ya kwanza timu ya Super Eagles kuchukua msimamo kama huo kuhusu fedha.


Mwaka uliopita walichelewa kufika katika michuano ya kombe la mashirika huko Brazil.