KIJANA ALIYEPOTEA KWA IMANI ZA KISHIRIKINA APATIKANA

Kijana mmoja mkazi wa kijiji cha Nyambogo wilayani Rorya mkoani Mara, ambaye anadaiwa kupotea nyumbani kwa imani za kishirikina hatimaye amepatikana huku akiwa katika hali ya kutisha bila kujitambua na mwili wake ukiwa umejaa tope jingi, tukio ambalo limevuta mamia ya wananchi wa kijiji hicho.

Kijana huyo Kenedy oguko mwenye umri wa miaka 22 amekutwa nje ya nyumba yao asubuhi ya Juni tano mwaka huku, akiwa uchi wa mnyama, ambapo baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wameiambia ITV kuwa tangu kutoweka kwa kijana huyo siku nne zilizopita, wamekuwa wakimtafuta bila mafanikio huku wakihusisha tukio hilo limefanywa kwa imani za kishirikina.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Rorya Bw Samwel Kiboye,ambaye ni miongoni mwa mashuhuda wa tukio hilo, amewaomba wananchi kuacha kulipiza visasi kwa kuwasaka watu wanaotuhumiwa kwa ushirikina bali watumie vyombo vya dola huku mwenyekiti wa kijiji hicho akilaani vikali vitendo hivyo vya ushirikina vinavyoendelea kijijini hapo hatua ambayo amesema imesabisha wananchi sasa kuishi kwa hofu kubwa.

Hata hivyo katika hali ya kushangaza wazee wa jadi kijijini hapo waliagiza kila mwananchi kupita mbele ya kijana huyo na kumpa mkono kama njia moja wapo ya kuwezesha kupata fahamu kitendo ambacho hata hivyo hakikuzaa matunda.


Chanzo: ITV