Mwishoni mwa wiki, mama mlezi wa Nasra, Josephina Joel, alisema hali ya mtoto huyo ilibadilika ghafla Mei 21 jioni, hali iliyosababisha madaktari waliokuwa zamu kumwekea mashine ya kumsaidia kupumua, ambayo alikuwa akiitumia mpaka karibu na mwisho wa maisha yake.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Ustawi wa Jamii mkoani Morogoro, Oswin Ngungamtitu, alisema kuwa mwili wa Nasra utasafirishwa leo kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwenda Morogoro na taratibu zote za maziko zitafanywa na Ofisi ya Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Ngungamtitu alisema kuwa kabla ya maziko, Nasra ataswaliwa katika Uwanja wa Jamhuri mkoani hapa badala ya nyumbani kwa mzazi wake, kwa kuwa baba mzazi wa mtoto huyo, Rashid Mvungi, ni mmoja kati ya washitakiwa wa kesi iliyofunguliwa mahakamani ya kulanjama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo.
Aidha taarifa ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, John Laswai, alieleza kuwa taratibu za kipolisi zitafanywa ikiwa ni pamoja na kupata taarifa ya daktari itakayoeleza sababu za kifo cha mtoto huyo.Taarifa hiyo kwa mujibu wa Kamanda Laswai, itapelekwa kwa wanasheria ambao wataipitia na kama itaonesha kuwa kifo cha Nasra kimetokana na ukatili na washitakiwa, basi Mvungi ambaye yuko nje kwa dhamana, atakamatwa na kesi itabadilika.
Miongoni mwa waliopokea msiba huo kwa simanzi wapo viongozi wa kata na mtaa aliokuwa akiishi mtoto huyo, pamoja na wadau mbalimbali ambao waliomba Serikali kuhakikisha maziko ya mtoto huyo yanafanywa mkoani Morogoro.
Tayari Mkurugenzi wa Kampuni ya mabasi ya Al Saed, Omary Al Saed, amejitolea usafiri wa kwenda Dar es Salaam kuchukua mwili na kuurudisha mkoani Morogoro kwa maziko na fedha taslimu Sh 400,000, kwa ajili ya gharama za dawa za kuhifadhi mwili pamoja nasanda.
Hata hivyo hatua ya Serikali kuamua swala kufanyika katika Uwanja wa Jamhuri, haikumfurahisha baba wa marehemu, ambaye katika kikao cha maandalizi ya maziko, alidai angefurahi kama angepewa mwili wa mtoto wake ili amzike mwenyewe badala ya kuzikwa na Serikali.
Mvungi alidai taarifa za kufariki dunia kwa mtoto wake huyo zimemchanganya na haijui cha kufanya, kwa kuwa tayari alishakaa na familia yake akiwemo mke wake na kukubaliana kumlea Nasra.
Katika makubaliano hayo kwa mujibu wa madai ya Mvungi, walikuwa wakisubiri apone ili wapeleke maombi Ofisi ya Ustawi wa Jamii, wapate ruhusa ya kumlea Nasra.
Alidai kuwa hakutarajia kwamba ndoto yake ya kumlea mtoto huyo tangu abainike kuishi kwa mateso katika boksi kwa zaidi ya miaka mitatu, ingeishia hapo lakini kwa mapenzi ya Mungu imetokea hivyohana njia ya kuzuia.
Nasra alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jumatano iliyopita kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, kwa ajili ya uchunguzi na tiba zaidi. Mama mlezi wa mtoto huyo hospitalini hapo, Josephine alisema:
"Nimesikitishwa sana, lakini ni Mungu ameamua kufanya kazi yake na hakuna anayeweza kupangua." Akiwa bado wadini, Josephine alisema mtoto huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia jana na kabla ya hapo alikuwa akijisikia vibaya na kusumbuliwa natumbo.
Msiba huo umetokea wakati Juni 9 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Morogoro, Mvungi na washitakiwa wenzake wakitarajiwa kufikishwa mahakamani hapo kujibu mashitaka ya kula njama na kufanya ukatili dhidi ya Nasra.
Washitakiwa wenzake Mvungi ni aliyekuwa mama mlezi wa Nasra, Mariamu Said (38) na mume wake,Mtonga Omar (30). Washtakiwa haowalifikishwa katika mahakama hiyo Jumatatu iliyopita chini ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo na kusomewa mashtaka hayo.
Wakili wa Serikali, Sunday Hyera alidai kuwa washitakiwa walitenda makosa hayo ya ukatili kati ya Desemba 2010 na Mei mwaka huu,katika mtaa wa Azimio Kata ya Kiwanja cha Ndege, mjini Morogoro.
Wakili huyo alidai kuwa katika wakati huo, washtakiwa wakiwa walezi wa mtoto Nasra, walimfanyia ukatili wa kumtelekeza na kumpa malezi akiwa ndani ya boksi na kumsababishia magonjwa.
Wakili huyo wa Serikali, alitaja maradhi yaliyomkumba mtoto huyo akiwa ndani ya boksi kuwa ni pamoja na utapiamlo, maumivu yakifua na mvunjiko wa mifupa katika mwili wake. Hyera alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba Mahakama kutaja tarehe ya kuisikiliza.
Chanzo: Habari leo