CARE INTERNATIONAL WATIMULIWA MTWARA

MKUU wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile, amelipa siku 14 Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Kimataifa la Care International Tanzania, kuondoka katika wilaya hiyo baada ya kubainika kuwa wanasambaza mbegu 'feki' za ufuta kwa wakulima.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Ndile alisema Care International walifika Mtwara kwa lengo la kufanya kazi na wanawake na wakulima vijijini, wakidai wanaongeza kipato cha wakulima kupitia ufuta.

Ndile alisema amechukua uamuzi huo baada ya kubaini kwamba shirika hilo linasambaza mbegu za ufuta aina ya Lindi 2003 ambazo ni feki, na tayari amemuagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), kuwafuatilia nyendo zao."

Nawapa siku 14 hatutaki kuziona ofisi zao hapa kwa sababu hawana mchango kwawana Mtwara… siwataki Care International katika wilaya yangu, nimepokea malalamiko ya wakulima wa Tarafa ya Mayanga na Mpapura wakisema kwenye mashamba yao kuna mbegu za ufuta zilizosambazwa mwaka 2013/2014 zinastawi vizuri, lakini hazitoi mavuno.


"Niliwaita wasaidizi wangu Idara ya Kilimo nikawauliza kuhusu Care, wakasema hawakushirikishwa, tumewauliza kituo cha Utafiti wa Mazao na Maendeleo Kanda ya Kusini, Naliendele nao hawakuambiwa… tumeliona suala hili ni zito, wanarudisha nyuma jitihada za maendeleo ya kilimo," alisema.

Mratibu wa Mradi wa Care International, Ofisi ya Mtwara, Morine Kwilasa, alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo alikuja juu akiwataka waandishi wa habari wampatie majina yao na vyombo wanavyofanyia kazi huku akibainisha kwamba si msemaji wa shirika hilo.