TBS WAKAMATA SHEHENA YA NGUO ZA NDANI

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekamata shehena ya marobota ya nguo za ndani za mitumba ambazo thamani yake haijajulikana kwa kuwa zimechangaywa na nguo za watoto.
Mkaguzi wa TBS, Donald Manyama alisema wamefanikiwa kukamata nguo hizo juzi bandarini zikiwa kwenye kontena mbili ambapo walilazimika kuongozana na wahusika ambao ni Kampuni ya Dema ili kuufanyia ukaguzi zaidi mzigo huo.
“Katika ukaguzi wetu , tumebaini kwamba marobota haya yanaonekana kama ni nguo za watoto lakini ndani kuna nguo nyingi za ndani za kike na za kiume za wakubwa na watoto za mitumba ambazo zimepigwa marufuku kuingizwa au kuuzwa nchini,” alisema.
Akiwa katika ghala za kampuni hiyo eneo la Mwenge, Dar es Salaam, Manyama alisema kazi ya kuzichambua na kuzitenganisha inaendelea ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Mfanyabiashara Mussa Kassim wa Kampuni ya Dema katika utetezi wake amedai  kusikitishwa kwake na hali hiyo hasa kwa kuwa wao waliagiza nguo za watoto na siyo za ndani kama ilivyotokea.
“Mitumba hii sisi tunaiagiza kutoka Ujerumani. Hatukuagiza nguo za ndani kwa kuwa siyo kusudio letu wakati Serikali imepiga marufuku. Nafikiri zimechangaywa kwa bahati mbaya,” alisema Kassim.