MWENYEKITI WA CCM AUWA KINYAMA

Watu wanadhaniwa kuwa ni majambazi wamemuua kinyama kwa kupiga risasi moja ya kichwani mwenyekiti wa chama cha mapinduzi kata ya Busambala wilayani Butiama mkoani Mara Bw Willison Opio mwenye umri wa miaka 6o huku kichwa chake kikisambaratishwa kabisa na risasi hiyo.

Mauaji hayo ya kinyama yamefanyika saa saba usiku wa kuamkia leo, baada ya majambazi hayo kuvunja milango ya nyumba aliyokuwa amelala kiongozi huyo na familia yake katika kijiji cha Kwikuba kabla ya kumshambulia kwa bapa za panga mke wamarehemu Bi Agness Wambura ambaye alilazimika kuwapa kiasi cha shilingi laki nne ambazo alizikopa kutoka katika taasisi moja ya fedha.

Afisa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Mara Acp Rogati Mlashan,akizungumza akiwa eneo la tukio, amesema baada ya majambazi hayo kuvunja milango miwili ya nyumba hiyo, walipiga risasi tatu na moja kumpata kichwani kiongozi huyo wa CCM na kufariki dunia papo hapo na kusema kuwa jeshi la polisi litafanya kila liwezavyo ili kuhakikisha wote walihusika kufanya uhalifu huo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Kwa upande wao baadhi ya viongozi serikali katika kata ya Busambala,wakizungumzia tukio hilo pamoja na kuonyesha masikitiko yao baada ya kupata taarifa za kifo cha kiongozi huyo wa CCM, wameliomba jeshi la polisi kuendesha msako mkali ambao utawesha kukamatwa kwa wahusika, hatua ambayo wamesema itasaidia kuondolea wananchi hofu kubwa waliyonayo sasa.