SHEKHE WA MKOA MAHAKAMANI

SHEHE wa Mkoa wa Tabora, Salum Shaban na waumini wengine watano wa dini ya Kiislamu, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka ya kutishia kufanya fujo.


Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Tabora, Issa Magoli, ilidaiwa na Wakili wa Serikali, Juliana Changalawe kwamba watu hao walitenda kosa Juni 14 mwaka huu katika Msikiti Mkuu wa Mkoa, ulioko eneo la Gongoni, mjini Tabora.

Washitakiwa wengine ni Mgude Ahmed, Said Maganga, Kassim Shomary, Abubbakar Ludenga na Kassim Rajab, wanaodaiwa kwamba siku hiyo mchana, walimtoa sehemu ya ibada Shehe Ibrahim Mavumbi.

Washitakiwa hao ambao wanawakilishwa na Mwanasheria Mussa Kwikima wa mjini Tabora, walikana mashitaka. Kesi iliahirishwa hadi Juni 30 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kutokana na upelelezi kukamilika.


Wote walipata dhamana. Kukamatwa hadi kufikishwa mahakamani kwa watu hao, kunatokana na mgogoro uliokuwa ukiendelea na kusababisha Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu, Issa Shaban bin Simba kutangaza kumuengua Shehe wa Mkoa wa Tabora, Shaban (mshitakiwa); kitendo ambacho kinapingwa na baadhi ya waumini.


Katika mgogoro huo, baadhi ya Waislamu wanapinga uamuzi wa Mufti kumtangaza Shehe Mavumbi Ally kuwa Kaimu Shehe wa Mkoa, wakidai alishindwa kwenye uchaguzi.