Utata wa kisheria umeibuka kuhusu utekelezaji
wa amri ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu kuhusu nafasi ya
mgombea binafsi nchini.
Juni 14, 2013, Mahakama hiyo ilitoa amri ya
kuitaka Serikali ya Tanzania kutoa taarifa ndani ya miezi sita kuhusu
hatua ilizochukua kulingana na hukumu hiyo.
Wakati wanasheria wakieleza kuwa kitendo cha
Serikali kushindwa kutekeleza amri hiyo kunaweza kuifanya nchi iwekewe
vikwazo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema
amri hiyo haiwezi kutekelezeka mpaka mchakato wa Katiba Mpya
utakapokamilika.
Akizungumza jana, Jaji Werema alisema nchi haiwezi
kuwekewa vikwazo vyovyote kwa kuwa tayari suala hilo lipo kwenye
mchakato wa Katiba Mpya na kama ikishindikana iliyopo itafanyiwa
marekebisho.
“Hakuna cha vikwazo wala nini… hilo suala kwa sasa
liko kwenye mchakato wa Katiba unaoendelea, hatuwezi kurekebisha Katiba
tena kwa hilo. Mnapaswa kuelewa hizi Mahakama za kimataifa, utekelezaji
wa hukumu unategemea pia uwezo wa nchi husika. Sisi tuko kwenye
mchakato wa Katiba, hadi ipatikane, isipopatikana ndipo tutaleta
marekebisho. Mbona kuna marekebisho mengi tu yaliletwa lakini
yanasubiri?”
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema: “Nchi haiwezi
kutumia sababu zake za ndani ya nchi kama kisingizio cha kutotekeleza
masharti ya mkataba iliyoridhia yenyewe kwa hiari na kwa nia njema.”
Mwanasheria kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika
(TLS), Steven Msechu alisema japo Mahakama ya Afrika ya Haki za
Binadamu haina jeshi la kuilazimisha Serikali kutekeleza hukumu hiyo,
bado itabanwa katika vikao vya nchi za Umoja wa Afrika... “Mahakama hiyo
itapeleka ripoti kwenye Baraza la Marais wa Umoja wa Afrika kuonyesha
kuwa Tanzania imeidharau... Baraza la Mawaziri wa Afrika nalo litapewa
taarifa kama hiyo, hivyo marais na mawaziri husika watahojiwa kwa nini
wameshindwa kutekeleza.”
Hata hivyo alisema Serikali inaweza kujitetea kuwa imeshaliweka suala hilo kwenye Rasimu ya Katiba hivyo liko kwenye mchakato.
Mchungaji Mtikila, TLS na LHRC walishinda kesi
hiyo waliyofungua katika Mahakama hiyo baada ya kushindwa katika rufaa
iliyofunguliwa na upande wa Serikali kupinga suala la mgombea binafsi.
Katika hukumu iliyosomwa na Rais wa Majaji wa
mahakama hiyo, Sophia Akuffor Arusha hivi karibuni, Serikali italazimika
kutekeleza kwa vitendo hukumu hiyo.