LOWASSA, MBOWE WAIKOSOA SERIKALI

KIONGOZI Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, wameikosoa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, wakisema kuwa ajira kwa vijana ni bomu linalofanyiwa mzaha.

Hii si mara ya kwanzakwa Lowassa kuinyooshea kidole Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), japo mara zote amekuwa akibezwa kuwa anatumia turufuhiyo kujijenga kisiasa wakati suala hilo si kubwa kiasi hicho.


Katika kampeni za kuingia madarakani mwaka 2005, Rais Kikwete aliahidi kutengeneza ajira milioni mbili kwa vijana, ahadi ambayo hadi sasa utekelezaji wake unatia shaka, kutokana na muda wake kufikia ukingoni.

Akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15 bungeni juzi, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, alisema suala la ajiralinapaswa liwe hoja maalumu bungeni kwa kuwa serikali imeshindwa kulipa kipaumbele.


Alisema ukosefu ajirani janga la kitaifa, serikali haionekani kushitushwa nalo na badala yake imekuwa ikifanya mikatati inayoishia ngazi za juu.

Mbowe alifafanua kuwa jambo hilo linatakiwa liwekewe mikakati kuanzia ngazi za halmashauri, mikoa na serikali kuu.

Alibainisha kuwa kuongeza ajira si suala la kufumania bali ni mkakati maalumu unaoandaliwa na serikali.


Alisema tukio lililotokea hivi karibuni jijini Dar es Salaam kwa vijana 11,000 waliokwenda kufanya udahili wa kupata nafasi 70 za ajira za Idara ya Uhamiaji, ni ishara mbaya kwa mwelekeo wa taifa.

"Serikali haipo makinina ukosefu wa ajira, na sisi wabunge hatulichukulii jambo hilo kwa ukubwa wake, vijana 11,000 wanawania nafasi 70! Hii ni hatari," alisema.


Aliongeza kuwa suala hilo limezungumzwa na watu wengi, akiwemo kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM, lakini akaelezwa si kubwa kama anavyolizua.Mbowe alisema tatizola ukosefu wa ajira limechangiwa na mfumo uliopo sasa wa kila kitu kurundi kwa kwenye Serikali Kuu.

Alisema tatizo hilo lingepungua kama halmashauri zingekuwa na mkakatiwa kuzitengeneza kwenye mazingira wanayofanyia kazi.

"Sioni haja ya kuwa nawataalamu wa uchumi na wakurugenzi katika halmashauri kama hawawezi kutengeneza ajira…. Tutengeneze mfumo wa ajira kuanzia ngaziza chini, serikali itoe agizo kwa halmashauri kutengeneza ajira," alisema.

Kwa mujibu wa Mbowe, miradi ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma (PPP) inaweza kulifanya taifa litengeneze kati ya sh bilioni 500 hadi 800.


*Madeni ya serikali

Kuhusu madeni, Mbowe alisema baadhi ya madeni ya taifa yanatokana na uzembe wa mawaziri na watendaji serikalini.

Kauli hiyo ameitoa juzi jioni bungeni alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015.


Mbowe alisema serikali imeliingiza taifa hasara ya sh bilioni tano kutokana na kushindwa kuilipa kwa wakati kampuni inayojenga bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Alisema ana barua za kutoka katika kampuni ya kujenga bomba la gesi ambayo inakwenda katika Shirika la Umeme na Wizara ya Fedha inayodai sh bilioni 5 kama riba na mkopo.

Kwa mujibu wa Mbowe, serikali haijailipa kampuni hiyo tangu Januari mwaka huu, kama mkataba unavyosema, hivyo kuzua hofu ya kukamilika kwa wakati kwa mradi huo."

Jamani madeni mengi ni ya kujitakia tu… ni uzembe tu hapa, tumeingizwa kwenye deni la sh bilioni tano kwa sababu ya wizara imeshindwa kuilipa kampuni hii.

"Tuna kila sababu kuangalia deni hili la taifa linasababishwa na nini ili tuangalie namna bora ya kulishughulikia na kuwashughulikia wale wote wazembe," alisema.


*Lowassa aibuka

Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli kupitia CCM, katika mchango wake alisema mara kwa mara alikuwa akitahadharisha kuwa ajira ni bomu, lakini watu hawakumuelewa.

Alisema sasa bomu hilo linaanza kupasuka taratibu na kuwa serikali inatakiwa kutengeneza ajira kwa vijana.


Kwa mujibu wa Lowassa, idadi ya Watanzania ni milioni48 na kila mwaka wahitimu wa vyuo vikuu wanafikia zaidi ya 40,000, lakini hakuna ajira.

Alisema ni lazima taifa liwe na mkakati wa kitaifa wa kuwasaidia vijana kwa kutengeneza ajira.


Lowassa aliongeza kuwa ujenzi wa kiwanda chochote ni vema ukaangalia utazalisha ajira kwa kiwango gani.

Alibainisha kuwa Rais Barak Obama wa Marekani, ni miongoni mwa viongozi walioingia madarakani kwa awamu ya pili baada ya kutengeneza ajira.


Chanzo: Tanzania Daima