Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Ofisa Mtendaji Kata ya Namatutwe, Salumu Mapunda alisema kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia juzi katika Kijiji cha Msikisi umbali wa mita 15 kutoka nyumbani kwa marehemu alikokuwa akiishi na familia yake.
Alisema kwamba kwa siku za hivi karibuni Njiliwi hakuwa na mahusiano mazuri na mke wake mara baada ya kuhisi kuwa kuna mwanamume ana mahusiano ya kimapenzi na mkewe.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji huyo alisema kuwa baada ya kugundua hilo Njiliwi aliamua kumpa talaka mke wake lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida mama huyo alikataa kuondoka nyumbani hapo kwa madai kwamba hawezi kuishi peke yake bila ya mume wake.
Mtendaji huyo aliendelea kueleza kuwa maisha yaliendelea kuwa magumu yasiyokuwa na maelewano kati ya wanandoa hao.
Mapunda alisema baada ya Njiliwi kuondoka nyumbani hapo watoto wake walianza kuingiwa na hofu kwani hata ilipofika jioni hawakumuona nyumbani na ndipo walipoamua kutoa taarifa kwa babuyao pamoja na majirani ambao pia walikiri kutomuona.
Alisema kuwa wakati jitihada za kumtafuta zinaendelea mke wake aliona mtu akiwa nyuma ya nyumba yao akiwa ananing'inia kwenye mti wa mkorosho na aliposogea kwa karibu alibaini kuwa ni mume wake amejinyonga ndipo alipotoa taarifa Ofisi ya Mtendaji Kata.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Zelothe Steven amethibitisha kutokea kwa tukio na kueleza kuwa wanandoa wanapaswa kuishi kwa amani.