Katika kesi hiyo iliyovuta umati mkubwa wa watu, waliojaribu kuwapiga washtakiwa hao kabla ya jaribio lao kuzimwa na polisi, hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro, Mary Moyo, ameridhia washtakiwa hao, Mariam Said, Mtonga Omary na Rashid Mvungi, warudishwe upya kituo kikuu cha polisi Morogoro kwa mahojiano ya awali, kama walivyoshauri waendesha mashtaka watatu wa serikali, Sunday Hyera, wakili wa serikali Edgar Bantulaki na inspekta wa polisi Zablon Msusi, na kesi hiyo ifikishwe tena mahakamani hapo Juni 12 kwa ajili ya kutajwa, na kwamba baada ya mahojiano washtakiwa hao warudishwe mahali husika kwa mujibu wa hati zao.
Washtakiwa hao wameondolewa na polisi kwa gari ndogo binafsi, iliyozungukwa na umati mkubwa wa watu, wengi wao wakiwa ni kina mama, ambao waliwazomea washtakiwa hao, na kusukuma gari yao huku wakiikimbiza kuelekea kituo cha polisi, na kila mmoja akirusha maneno ya kuwatuhumu washtakiwa hao.
Katika maelezo ya awali ya mashtaka, washtakiwa hao wamedaiwa kula njama na kumfanyia ukatili mtoto huyo, ambaye mama yake mzazi alifariki dunia na jukumu la malezi kuachiwa mama yake mkubwa ambaye ni mshtakiwa wa kwanza, kwa kumfungia kwenye boksi na kumyima huduma za msingi, ikiwemo chakula, tiba, mavazi na malazi, hali iliyosababisha apate ugonjwa wa nimonia, utapiamlo, maumivu ya kifua na kuvunjika kwa mifupa ya miguu na mikono.