WANAFUNZI DIT WAENDELEA NA MGOMO

Polisi jijini Dar es Salaam wamelazimika kufunga barabara ya jamhuri iliyopo katikati ya jiji kwa saa kadhaa baada ya wanafunzi wa taasisi ya teknolojia Dar es Salaam DIT kuandamana kwenda wizara ya sayansi na teknolojia kwa nia ya kuonana na waziri husika ili kufikisha kilio chao juu ya wanafunzi zaidi ya mia sita waliozuiwa kufanya mitihani.

Ikiwa ni siku ya pili ya mgomo wa wanafunzi hao kutokuingia kwenye vyumba vya mitihani kama sehemu ya kushinikiza uongozi wa chuo hicho kuwaruhusu wenzao 684 waliozuiwa kufanya mitihani kutokana na kutokumalizia ada ambapo licha ya polisi kuwazuia lakini walifanikiwa kufika nje ya jengo la wizara hiyo.

Rais wa serikali ya wanafunzi Emida Elihuruma amesema wamefikia uamuzi wa kuandamana baada ya kuona kuwa uongozi wa chuo umeshindwa kutatua mgogoro huo licha ya wao kufuata taratibu zote.

Jitihada za ITV kuupata uongozi wa chuo hicho kuzungumzia suala hilo zinaendelea baada ya kuelezwa kuwa viongozi wako kwenye kikao, ambapo ITV imefika chuoni hapo na kushuhudia askari wa kikosi cha kuzuia ghasia wakiwa wameimarisha ulinzi baada ya wanafunzi hao kurudi ndani ya chuo wakimsubiri katibu mkuu wa wizara ya sayansi na teknolijia ambaye aliwaahidi kwenda kuzungumza nao.

Chanzo:ITV