Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwasili Dodoma keshokutwa,
ikiwa ni siku moja kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali kwa
mwaka wa fedha 2014/15.
Habari zilizopatikana jana zinasema Rais ataongoza
kikao cha Baraza la Mawaziri kitakachopewa muhtasari kuhusu Bajeti ya
Serikali ya mwaka ujao wa fedha na baadaye atafuatilia uwasilishaji wa
bajeti hiyo bungeni akiwa Dodoma.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu
alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yuko likizo lakini
akaweka bayana kwamba kwa kawaida kabla ya bajeti kuwasilishwa bungeni,
lazima Baraza la Mawaziri lipewe muhtasari wa bajeti husika.
“Ni kawaida kabla ya bajeti kuwasilishwa, Rais
huongoza kikao cha Baraza la Mawaziri yaani pre budget cabinet meeting
ambako Waziri wa Fedha hutoa briefing (muhtasari) kuhusu maeneo muhimu
ya bajeti, kwa hiyo siyo jambo jipya ni suala la kawaida,” alisema
Rweyemamu.
Itakumbukwa kuwa mwaka jana kabla ya kusomwa kwa
bajeti ya 2013/14, Rais Kikwete alikuwa Dodoma ambako pamoja na kukutana
na mawaziri, pia alifanya kikao na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Hata hivyo, uwepo wake mjini Dodoma safari hii
umekuja wakati kukiwa na dalili za mvutano mkubwa kati ya Bunge na
Serikali kutokana na kutotolewa kwa fedha za kutosha za maendeleo kwa
mwaka wa fedha unaoisha Juni 30 mwaka huu.
Taarifa zinasema bajeti inayomalizika mwishoni mwa
mwaka huu, inapungukiwa kiasi cha Sh1.8 trilioni, huku Serikali
ikilaumiwa na wabunge kwa kutoa misamaha ya kodi inayofikia Sh1.52
trilioni, ambayo ingepunguza nakisi iliyopo kwenye bajeti kwa asilimia
84.4.
Wakati wa mjadala wa bajeti za wizara tangu kuanza
kwa Bunge la Bajeti Mei 6 mwaka huu, wabunge wamesikika mara kadhaa
wakilalamika kwamba fedha za maendeleo zilizotolewa kwa wizara katika
bajeti ya 2013/14 ni kati ya asilimia 25 na 30, jambo ambalo
limesababisha kukwama kwa miradi mingi.
Keshokutwa itakuwa siku ya mwisho ya mashauriano
baina ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Bunge kupitia Kamati yake
ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Mazungumzo hayo yaliyoanza Juni 5 mwaka huu,
yalilenga kuangalia uwezekano wa kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili
kuwezesha kuzingatiwa kwa ushauri wa wabunge, pamoja na kusaka fedha
kuziba pengo la Sh1.8 trilioni katika bajeti ya 2013/14.
Alipoulizwa jana, Chenge hakuwa tayari kuzungumzia
hatua iliyofikiwa katika mashauriano hayo na badala yake alisema kwa
ufupi: “Ndugu yangu mambo ya Bunge, tutakutana kwenye taarifa yetu ya
kamati tutakayoiwasilisha bungeni.” Kamati ya Bajeti katika maoni yake
iliyoyatoa Juni 17 mwaka jana kuhusu Bajeti ya Serikali ya 2013/14,
iliweka bayana kuwapo kwa udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato,
baadhi ya wizara kutumia fedha nyingi kuliko ilivyoidhinishwa na Bunge
na Serikali kuwa na matumizi makubwa kuliko mapato yake.
Sehemu ya taarifa hiyo iliyosomwa na Chenge
ilibaini kuwa katika bajeti ya 2011/12 Serikali ilitumia kiasi cha Sh1.3
trilioni ya mapato yake na mwaka wa fedha uliofuata 2012/13 ilizidisha
kiasi cha Sh1.5 trilioni.
“Hali hii imesababisha Serikali kuendelea kukopa kutoka nje na
ndani kwa ajili ya kufidia pengo la upungufu wa fedha. Kamati imebaini
kuwa kuendelea kukopa ambako hakuendi sambamba na juhudi za ukusanyaji
wa mapato, kutaendelea kuwa mzigo kwa nchi kwani itaendelea kukopa na
kuongeza kiasi cha matumizi,” inasomea sehemu ya taarifa hiyo.
Mashauriano
Habari zilizopatikana kutoka Dodoma zinasema vikao
vya majadiliano baina ya Serikali na Bunge vinaendelea leo baada ya
kusitishwa Jumamosi saa tano usiku, huku kukiwa na mjadala mkali kuhusu
uwezekano wa kupatikana kwa fedha za kutekeleza bajeti inayofikia ukomo
wake mwezi huu.
“Kwa kweli mvutano umekuwa mkali kati ya Waziri wa
Fedha na watendaji wa wizara hiyo kwa upande mmoja, dhidi ya wajumbe wa
Kamati ya Bajeti kwa upande mwingine. Kubwa ni kutizama vyanzo vipya
vya mapato,” kilidokeza chanzo chetu.
Habari zinasema katika kikao kilichofanyika
Ijumaa, hoja iliyotawala ilikuwa ni kutafutwa kwa vyanzo mbadala vya
mapato na wajumbe wa kamati hiyo waliibana Serikali wakiitaka iondokane
na utamaduni wa kutoza fedha kutoka kwenye soda, bia, maji na sigara
pekee.
Hata hivyo, wiki iliyopita Spika wa Bunge, Anne
Makinda alisema katika kikao hicho cha Kamati ya Bajeti na Serikali
hakuna fedha zitakazoongezwa na kitakachofanyika ni kutoa fedha kutoka
eneo moja na kupeleka eneo jingine lenye umuhimu na uharaka katika
utekelezaji wake.
Miongoni mwa maeneo ambayo wabunge wanaitaka
Serikali kuongeza fedha ni sekta ya maji ambayo inapendekezewa iundiwe
mfuko wa maji vijijini ili kuikabili kero hiyo ambayo imekuwa na athari
kubwa kwa wananchi.
Shinikizo la wabunge kuhusu suala la mfuko wa maji
limekuja wakati Wizara ya Maji hadi sasa ikiwa inahitaji kupewa kiasi
cha Sh126 bilioni ambazo ziliidhinishwa katika bajeti ya 2013/14.
Katika kujaribu kupunguza nakisi hiyo, Serikali
ilikubali kutafuta kiasi cha Sh100 bilioni kabla ya mwaka huu wa fedha
kumalizika ili zielekezwe katika miradi ya maji na taarifa zinasema
tayari imetoa Sh80 bilioni.
Wakati wa mjadala wa Wizara ya Afya, wabunge pia
walichachamaa wakikosoa hatua ya kupunguzwa kwa kiasi cha Sh131 bilioni
ikilinganishwa na mwaka wa fedha unaomalizika na kwamba punguzo hilo
litaathiri kwa kiasi kikubwa tiba na huduma za afya nchini.
Mwaka ujao wa fedha, wizara hiyo imeidhinishiwa
Sh622 bilioni, ikilinganishwa na kiasi cha Sh753 bilioni
zilizoidhinishwa 2013/14.
Wizara ya Uchukuzi nayo ilikuwa na wakati mgumu
wakati wa mjadala wa makadirio yake ya matumizi, pale wabunge
walipochachamaa wakitaka fedha ziongezwe kwa ajili ya Shirika la Ndege
(ATCL), ukarabati wa meli ya MV Victoria na upanuzi wa Uwanja wa Ndege
wa Mwanza.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi