KOBE WAZUA TAHARUKI DAR

HALI ya taharuki ilizuka jana katika eneo la Tabata Mawenzi jijini Dar es Salaam baada ya kobe wadogo zaidi ya 300 kuonekana katika maeneo hayo huku wakiwa hawajulikani walipotokea.


Kobe hao walikutwa katika shamba la Hassan Msumi wakiwa wametapakaa eneo zima la shamba hilo kana kwamba kuna mtu alifika na kuwamwaga eneo hilo.


Akizungumzia tukio hilo, Msumi alisema jambo hilo linastaajabisha kwani ameishi katika maeneo hayo tangu miaka ya 1980 lakini hakuwahi kuona kobe hata mmoja.


"Inashangaza sana kwa sababu tangu tumeanza kuishi katika maeneo haya hatujawahi kuona kobe, tunajiuliza hawa wametokea wapi lakini hatuna jibu," alisema Msumi.


Msumi alisema asubuhi ya jana wakati baadhi ya watu wakienda kuchota maji katika kisima kilichopo ndani ya shamba hilo, mdogo wake wa kike aliwaona kobe hao na ndipo alipomuita ili aje kushuhudia.


Alisema wakati akijiandaa kutoka kuna muokota chupa za plastiki alikuwa anapita jirani na shamba hilo, baada ya kuwaona alimwaga chupa na kuanza kuwaokota kobe hao.


"Kuna 'teja' alikuwa anaokota chupa lakini alipowaona hawa kobe alimwaga machupa yake yote akaanza kuwaokota na wakati mimi natoka ndani alikimbia," alisema.

Alisema mtu huyo alifanikiwa kuondoka na kobe hao wakiwa wamefikia nusu ya kiroba hicho alichokuwa amekibeba.


Aliongeza kuwa walianza kuwakota kobe waliobaki na kuwakusanya sehemu moja ambapo idadi yao ilifikia 338 huku aliokimbia nao mtu huyo idadi yake ikiwa haijulikani.

Inasemekena alioondoka nao idadi yake inaweza kufikia 300.

Msumi alisema baada ya kuwakusanya kobe hao alichukua hatua ya kutoa taarifa kwenye Idara ya Wanyamapori ili waje kuwachukua baada ya baadhi ya vijana kuanza kuwapiga kwa mawe.


Hata hivyo Msumi alisema baada ya kobe hao kuchukuliwa, wengine walianza kuonekana mmoja mmoja ambapo watu wa eneo hilo walikuwa wakiwakusanya.


Wakazi wengi wa eneo hilo walikusanyika kuwashangaa kobe hao na kujiuliza walipotokea bila kuwa na majibu.


Ofisa mmoja wa Idara hiyo ya Maliasili ambaye alikataa kunukuliwa kwa kuwa si msemaji alisema, kitendo kilichofanywa na watu hao ni cha kiungwana kwani wangeweza kuwaficha na kutafuta wateja kwa ajili ya kuwauza.

Alisema kwa mujibu wa Sheria za nchini hairuhusiwi mtu kumiliki kobe ila ni mali ya serikali.


Kwa kawaida kobe jike huchimba kiota na kutaga mayai ndani yake nyakati za usiku na kufunika kwa udongo, mchanga au vitu vya organi ambapo hukaa kwa siku 60 hadi 120 na kutotolewa.


Kobe mmoja anaweza kutaga mayai kati ya moja hadi 30, na inasemekana kuwa kobe anaishi maisha marefu kuliko wanyama wengine, wapo wanaoishi maisha zaidi ya 150 .