KASHIFA YA RUSHWA YAZIDI KUIANDAMA FIFA

Madai mapya ya ufisadi yameibuka dhidi ya shirikishola soka duniani FIFA kuhusiana na utata uliosababisha taifa la Qatar kupewa rukhsa ya kuandaa michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2022.

Gazeti la Sunday Times kutoka Uingereza limesema kuwa limepata stakhabadhi zinazoonyesha ambavyo aliyekuwa afisa wa shirikisho la soka nchini Qatar Mohammed bin Hammam, aliwalipa mamilioni ya madola maafisa wa soka kwamadhumuni ya kuiunga mkono Qatar kuandaa michuano hiyo mwaka mmoja kabla ya uamuzi kutolewa.

Bwana Hammam amekataa kujibu madai hayo mapya.Lakini mwandishi wa michezowa BBC amesema kuwa huenda shinikizo zikatolewa dhidi ya FIFA kufanya kura mpya ya kuandaa michuano hiyo ya mwaka 2022.

Jarida la Sunday Times , lilifichua ambavyo mamilioni ya dola zilikabidhiwa maafisa wa shirikisho hilo kupitia kwa akaunti zao pamoja na kuwepo ushahidi wa barua pepe kuhusu mawasiliano yaliyokuwepo, shughuli hiyo ilipokuwa inafanyika.

Inaarifiwa Mohamed Bin Hammam aliwalipa dola milioni 5 maafisa wa FIFA ili waweze kuunga mkono Qatarwakati kura ya nchi itakayoandaa kombe la dunia2022 ilipofanyika.

Qatar imekanusha madai hayo.

Lakini kulingana na nyaraka zilizopatikana na Sunday Times na ambazo BBC imeweza kuona, ni bayana kuwa Bin Hammam, mwenye umri wa miaka 65, alianza kuwarai maafisa wa shirikisho hilo kupigia kura Qatar mwaka mmoja kabla ya kura yenyewe kufanyika.

Stakabadhi hizo zinaonyesha ambavyo, Bin Hammam alikuwa anawalipa maafisa wa soka barani Afrika ili kununua ushawishi wao waweze kuunga mkono Qatar.

Hata hivyo, Qatar imekanusha vikali madai hayo ikisema kuwa Bin Hammam hakuwahi kuwa na jukumu la kuunga mkono azma ya Qatar kutaka kuandaa kombe la dunia 2022 na kwamba hakuwa anapigia debe Qatar kivyovyote.