WAATHIRIKA WA DAWA ZA KULEVYA 563 WAJIPELEKA KLINIKI

JUMLA ya waathirika 563 wa dawa za kulevya katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida wamehudhuria kliniki katika kipindi cha mwaka jana.

Mratibu wa Afya ya Akili wa Manispaa ya Singida, Crescencia Mapunda alimwambia hayo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa , Rachel Kassanda wakati Mwenge ulipotembelea Shule ya Msingi Mtamaa ili kujionea moja ya juhudi za Manispaa hiyo kupambana na dawa za kulevya.

Katika kudhihirisha kuwa dawa za kulevya ni tatizo kubwa katika Manispaa ya Singida, Mapunda alisema kuwa kati ya Januari na Juni mwaka huu pekee kumekuwa na waathirika 208 na kwamba wanaothirika zaidi ni wale wenye umri kati ya miaka 12 na 45.

Hata hivyo alisema pamoja na kwamba dawa za kulevya ni tatizo kubwa Manispaa hiyo, takwimu za makosa hayo imeendelea kushuka kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Miaka hiyo na kesi zake kwenye mabano ni mwaka 2012 (123) , mwaka 2013 (97) wakati mwaka huu Januari hadi Machi kume kuwepo na kesi 25.

Aidha, alisema kuwa sehemu kubwa ya kesi hizo ni za bangi, mirungi na pombe haramu ya gongo wakati kesi za kokeni na heroini ni tatu.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Rachel Kassanda aliipongeza Manispaa hiyo kwa juhudi zake za makusudi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa elimu ya ufahamu wa madhara yaletwayo nadawa za kulevya kwa marika mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mapunda, Manispaa ya Singida ina jumla ya vituo vitatu vinavyo jishughulisha na kampeni dhidi ya dawa za kulevya na kuwasaidia waathirika kwa kuwapatia tiba maliwazo.