ARFI: JIMBO KWANZA, CHADEMA BAADAE

SIKU moja baada ya Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Amour Arfi (Chadema) kushangaza kambi ya upinzani kwa kupiga kura ya kuunga mkono Bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015, mwenyewe amesema amefanya hivyo kwa ajili ya jimbo lake na si kutanguliza maslahi ya Chama chake kama wafanyavyo wabunge wengine.


Arfi aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa na nafasi hiyo kujiuzulu mwaka huu, aliunga mkono bajeti hiyo akiwa ni miongoni mwa wabunge wanne waupinzani na kusababisha kushangiliwa kwa nguvu na wabunge wa CCM.


Wengine waliounga mkono Bajeti hiyo ambapo hata bajeti hii ya mwaka 2013/2014 inayomalizika waliiunga mkono na vyama vyao kwenye mabano ni Mbunge wa Vunjo Augustino Mrema(TLP), John Cheyo wa Bariadi Mashariki(UDP) na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed(CUF).


Katika bajeti hiyo inayoanza kutekelezwa Julai mwaka huu, wabunge 234 walipiga kura ya Ndiyo na wabunge 66 wakiikataa bajeti hiyo ya Sh trilioni 19.8. Wabunge 54 hawakuwepo bungeni.

Idadi kamili ya wabunge ni 357.


Akizungumza na gazeti hili jana baada ya kuulizwa sababu ya kwenda kinyume na kambi ya upinzani na kuwa Mbunge wa kwanza kuunga mkono Bajeti ya serikali, alitoa sababu kadhaa ambazo ni pamoja na kuridhishwa na serikali katika kutatua kero nyingi za jimboni kwake pamoja naWaziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum kutatua kero za muda mrefu.


"Nikiwa kama Mwakilishi nina mambo matatu makuu ya kusimamia pamoja na kuwasemea watu, la kwanza ni Jimbo langu, pili Nchi yangu na tatu Chama changu (Chadema).

Katika haya matatu kwa bajeti hii niliamua kwa ajili ya jimbo langu tofauti na wengi wanaotanguliza vyama vyao kuliko majimbo na nchi yao,"alitetea uamuzi wake wa kuunga mkono Bajeti hiyo.


Arfi ambaye anaamini kitendo cha kuunga mkono bajeti hiyo ni kudumisha utamaduni wa demokrasia kuchukua mkondo wake wa kukubaliana na kutokubaliana, alisema ameridhishwa na majibu yaliyotolewa na Waziri wa Fedha kwa maana alivyoweka bayana katika yale anayoamini ikiwemo misamaha ya kodi ambayo imekua kero ya muda mrefu.


"Pia utayari wake(Waziri) wa kujipunguzia mamlaka ya kutoa misamaha jambo ambalo watangulizi wake walishindwa. Pia kwa namna alivyohimiza ukusanyaji wa mapato na nidhamu ya Bajeti na hususan kukabiliana nawakwepa kodi na wale ambao wanadhani hawawezi wafunge biashara zao,"alifafanua.


Sababu nyingine ambazo ni majibu ya matatizo mengi ya jimbo lake lauchaguzi ni kuendeleza na kukamilisha mradi mkubwa wa Maji wa Ikolongo ambao tayari mabomba katika kilometa 46 yametandi kwa jambo ambalo anaamini litamaliza kabisa tatizo la Maji jimboni kwake na kuingizwa katika mpango wa serikali wa ujenzi wa barabara za lami kufungua Mkoa wa Katavi yaani Mpanda-Tabora na Mpanda-Kigoma.


Majibu ya matatizo mengine ni kuwepo kwa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Mkoa Mpanda Mjini, kuondoa tatizo la Umeme Mpanda kwa kupeleka jenereta mbili mpya na kupeleka umeme katika vijiji vyote katika jimbo lake pamoja na kuwepo kwa fedha kwa ajili ya reli ya Kaliua hadi Mpanda na mpango wa kuendeleza kazi hiyo hadi Karema.


Arfi alisema "utatuzi mwingine wa kero ni Mji wa Mpanda kuwemo katika Mpango wa Maendelezo ya Miji ambapo tutapata fursa nyingi, Mji kupimwa vyema na uwepo wa miundombinu bora katika Mji wa Mpanda".


Chanzo: Habari Leo