MABOMU YATIKISA TARIME

POLISI Kanda maalumu ya Tarime na Rorya Mkoa wa Mara, imelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya wananchi wenye hasira wa mji mdogo wa Sirari.


Wananchi hao walikuwa wakiandamana barabarani kwenda kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Sirari(OCD), huku wakichoma matairi ya magari wakidai polisi kituo cha Sirari wamemuua kwa kipigo mkazi mmoja wa Kitongoji cha Sokoni katika mdogowa Sirari.

Mkazi aliyeuawa alifahamika kwa jina Tandeka Mserega (25), ambaye niyatima.


Maandamano ya wananchi hao yalizimwa jana saa 7 mchana, ambapo maandamano yalianza saa 12 asubuhi.

Maandamano hayo yalisababisha shughuli mbalimbali za kimajii na kiuchumi kusimama kwa muda.

Wakizungumzia maandamano hayo,baadhi ya wananchi jana, walisema yametokana na tukio la Juni 17, mwaka huu, ambapo polisi wa Kituo cha Sirari walimkamata kijana huyo ambaye ni dereva wa bodaboda.


Walisema baada ya kumkamata walimpandisha kwenye kwenye gari la polisi na kuondoka naye kwenda kwenye kituo cha Polisi cha Sirari bila kujua tuhuma yake.


Mmoja wa ndugu zake marehemu,Mariam Kirigiti, alisema kuwa,walifuatilia kituo cha polisi asubuhi sikuya pili, lakini walimkosa ndugu yao.

"Hivyo, tuliamua kwenda Kituo Kikuu cha Polisi cha Tarime nagereza la Tarime, baada ya kushindwa kumpata,"alisema.


Aliongeza kuwa, walifanikiwa kupata taarifa kutoka kituo cha Polisi cha Sirari kwa askari mmoja kuwa, ndugu yao alifariki dunia na mwili wake ulihifadhiwa chumba cha maiti katika Hospitali ya Tarime.

Ndugu hao walitaka kujua kifo chandugu yao, kwani wakati akikamatwa na polisi, alikuwa mzima na hakuwa na tatizo lolote kiafya.


Walidai kuwa, hawakupata majibuya kuridhisha kutoka kwa polisi wakituo hicho, Hivyo waliamua kuweka msimamo hadi waelezwe ukweli.


Msimamo huo, uliwafanya wananchi wa Sirari kuamua kufanya maandamano kwa jazba ya kufunga barabara, kuchoma matairi na kurusha mawe yaliyosababisha baadhi ya polisi akiwamo mkuu wa upelelezi wa kituo hicho kukutana na adha ya mawe hayo.