ZIARA YA DK. SLAA YAAHIRISHWA KIGOMA

KITENDO cha kuwavua uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe na aliyekuwaMjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo, kimesababisha ziara ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa mkoani Kigoma, iahirishwe.

Hatua hiyo imefikiwa na uongozi waChadema Mkoa, baada ya kupata taarifa za mipango haramu ya kusababisha uvunjifu wa amani wakati kiongozi huyo atakapokuwa mkoani Kigoma. Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Kigoma, Jafari Kasisiko, alisema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari, alipokuwa akizungumzia kusitishwa kwa ziara hiyo.

Kasisiko alisema wameandika baruakwenda Makao Makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam, kuomba kuahirishwa kwa ziara hiyo ya Dk Slaa kwa kile ambacho uongozi wa Mkoa unaona hauna uwezo wa kudhibiti hali hiyo, iwapo itatokea.

Kabla ya kuomba kuahirishwa kwa ziara hiyo, Mwenyekiti huyo alisema Baraza la Ushauri la Mkoa Kigoma, lilikaa na kupokea taarifa kutoka kwa viongozi wa majimbo mbalimbali ya mkoa, zilizoonesha wapenzi wengi wa Chadema katika maeneo hayo, hawako tayari kumpokea Dk Slaa.

Alisema viongozi wengi waliohudhuria kikao hicho cha ushauri, walieleza kuwa maeneo yao kwa sasa hawako salama kumpokea kiongozi huyo wa kitaifa, kutokana na kuendelea kwa vitendo vya baadhi ya wanachama kuchoma bendera na kuharibu matawi ya chama hicho.

Alitoa mfano wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, ambako vurugu ni kubwa zaidi na taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa iwapo Dk Slaa atafika maeneo hayo, wanachama na baadhi ya wapenzi wa chama hicho, wamepania kumfanyia vurugu mbalimbali, ambazo mwisho wake siyo mzuri kwa chamahicho.

Pamoja na hali hiyo, Mwenyekiti huyo wa Chadema Mkoa Kigoma, alisema ziara hiyo ya Katibu Mkuu haina uhusiano wowote na hatua ya Kamati Kuu ya Chadema kumvua uongozi Naibu Katibu Mkuu huyo, na kwamba viongozi wa chama hicho mkoani humo wanaunga mkono hatua iliyochukuliwa na Kamati Kuu.

Katibu Mkuu wa Chadema alitarajiwa kuanza ziara ya kuimarisha chama mkoani Kigoma Desemba 5 mwaka huu, ambapo alitarajiwa kuzunguka majimbo yoteya uchaguzi mkoani Kigoma na kuhitimisha ziara hiyo Desemba 13 mwaka huu.

Gazeti hili lilitafuta viongozi wa Chadema makao makuu, ambapo simu zao zilikosekana. Baadaye mmoja wa maofisa aliyekuwa mstari wa mbele kutoa taarifa kuhusu yanayojiri baada ya ya akina Zitto kung'olewa madaraka, alisema maandalizi ya ziara hiyo yanaendelea. "Leo ndiyo mmepiga simu ili kufanya uwiano, siku zote mnaandika habari za umbeya, hamjawahi kupiga simu.

Leo imekuwaje?," alisema ofisa huyo, ambaye alikuwa mstari wa mbele kutoa namba za wasemaji wa kutetea hatua ya Kamati Kuu.

"Kwa taarifa yako sasa, tayari huko Kigoma watu wanafanya maandalizi makubwa ya kumpokea Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa, wewe unafikiri huo ni uamuzi wa mtu mmoja tu, hiyo ni lazima vikao vikae ndiyo viahirishwe. "Mpaka sasa ninapoongea na wewe hapa, maandalizi ni makubwa sana, naomba usininukuu mimi. Nakutumia namba za watu ambao watakupa habari kamili ambao wapo huko Kigoma," alisema na baadae kutoa namba hiyo.

Hata hivyo, baadae namba hiyo ilipotolewa, haikupatikana.


Habari Leo