RAIA WAWILI WA UFARANSA WAUWAWA NA KUTUPWA KISIMANI HUKO ZANZIBAR

Raia wawili wa Ufaransa wameuawa na kutumbukizwa katika kisima cha maji kilichomo ndani ya uwanja wa nyumba yao na watu wasiojulikana katika eneo la Shehia ya Matemwe Kaskazini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Yussuf Ilembo zinaeleza kuwa watu hao mtu na mkewe waliuawa hivi karibuni.

DCI Ilembo aliliambia gazeti hili jana kuwatayari vikosi vya Zimamoto na Uokozi (KZU) na Polisi vimeanza kufukua kisima hicho na kwamba katika hatua ya awali wamefanikiwa kukuta mfupa wa mguu wakushoto wa mmoja wa watu hao.

Aliwataja wazungu hao kutoka Ufaransa kuwa ni Francois Cherer Robert Daniel na Brigette Mary ambao walikuwa wakiishi kama mtu na mkewe wakiwa na mbwa wao anayeitwa Allan ambaye pia amekutwa amekufa ndani ya nyumba hiyo.

Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa Wafaransa hao waliingia nchini kihalali mwaka 2013, na kununua nyumba kwenye ufukwe wa mwambao wa Bahari ya Hindi eneo la Matemwe na kuanza kuishi eneo hilo.

DCI Ilembo alisema polisi tayari wanawashikilia watu watatu wakazi wa Shangani katika Mjimkongwe wa Zanzibar na mmoja anayeishi katika eneo la Kilimani katika wilaya ya Mjini Unguja.

"Kuna askari wanaendelea na kazi ya kuzamia ndani ya kisima kilichomo ndani ya uzio wa nyumba hiyo, kazi bado ni kubwa na siyo ya siku moja," alisema DCI Ilembo.


Gazeti hili limefanikiwa kufika katika eneo la nyumba hiyo na kukuta askari Polisi wanne wakilinda nyumba hiyo huku harufu kali ikitoka katika shimo la kisima.

Hata hivyo, mlinzi wa nyumba hiyo ametoweka katika mazingira ya kutatanisha na simu yake kila ikipigwa imezimwa.

Mlinzi mpya aitwaye Omar Juma ambaye amekutwa akilinda nyumba hiyo baada yakuajiriwa na mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa amesema alikabidhiwa kazi ya ulinzi kuanzia Januari mwaka huu na hakumkuta mtu yeyote akiishi hapo.

"Kazi yangu ni kazi za ulinzi, nimeletwa hapa na mwajiri, sijui lolote, mwajiri wangu ndiye anayejua kama kulikuwa na watu kabla au la, sina la kusema na sijui nianzie wapi," alisema Omar.

Sheha wa Matemwe KusiniSheha wa Shehia ya Matemwe Kusini, Denge Khamis Silima aliyelizungumzia suala hilo kwa niaba ya Sheha wa Matemwe Kaskazini, aliliambia gazeti hili kuwa taarifa za kutoweka kwa wazungu hao zilianza kuenea kuanzia Desemba 27 mwaka jana.


Denge alisema alianza kupata taarifa za awali kutoka kwa mjumbe mmoja wa Shehia aitwaye Mkadam Tabu Vuia kwamba mlango wa nyumba ya wazungu hao ulikuwa wazi kwa muda mrefu na harufu kali ikitoka na inzi wakubwa wametanda katika eneo hilo.

"Nimeshiriki katika kazi ya kuchimbua kisima, askari wametoa mfupa wa mguu na unyayo unaoaminika kuwa ni wa mtu, ingawa tuliikuta nyumba ikiwa haikuvunjwa milango," alisema.

Alisema waliingia ndani ya nyumba hiyo kupitia dirishani wakakuta mbwa wa wazungu hao, Allan naye amekufa na kwamba kwa sasa wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa polisi.


Sheha huyo wa Shehia ya Matemwe Kusini alisema mazingira waliyoyakuta ndani ya nyumba hiyo yameonyesha kuwa haikuhamwa kwa muda mrefu na kama kwamba wanatarajia kurejea wakati wowote.


Alisema baada ya kutoa taarifa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya, askari polisi walifika katika eneo hilo na kazi ya kuchimba kisima ilianza baada ya kubaini harufu kaliilikuwa inatoka kisimani.

Hata hivyo, kazi ya kuchimba kisima ilikuwa ngumu baada ya kukutana na zege lililojazwa na walipoendelea kuliondoa zege hilo walipata mguu mmoja wa binadamu.

Denge alisema zoezi la uchimbaji wa kisima hicho lilikwama juzi kutokana na ugumu wa zege na hivyo kazi hiyo kuahirishwa na kuendelea jana baada ya kupatikana mashine ya kuchimbua vitu vigumu na vifaa ya kuongeza hewa ya oksijeni.


"Bado hatujafanikiwa kubomoa zege na kuingia kina kirefu kujua kama ipo mifupazaidi au la, tunawasubiri polisi na askari wa zimamoto waje na vifaa," alisema Denge.

Agosti 7, mwaka jana raia wawili wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18) walimwagiwa tindikali mjini Zanzibar.

Tukio hilo lilitokea saa 1:15 usiku Mtaa wa Shangani eneo la Mji Mkongwe wa Zanzibar, karibu na ofisi za Serikali ikiwamo Wizara ya Sheria na Wizara ya Katiba na Maendeleo ya Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto.

Wasichana hao walifika Zanzibar kwa mwaliko wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Arts in Tanzania.


Chanzo:- Mwananchi