Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema jana kuwa silaha hizo zilizokuwa chini ya Mamlaka yaMapato Tanzania (TRA), tangu Novemba 2012 kutokana na kutokulipiwa kodi, zitasambazwa Ngorongoro, Selous, pamoja na Hifadhi za Taifa za Tanapa.
Kati ya silaha hizo, 250 zitapelekwa Idara ya Wanyamapori, 200 Tanapa na 50 Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro.
"Silaha hizi jumla ya Sh427 milioni kuzinunua lakini zilikwama TRA kwasababu ya kutolipiwa kodi na ushuru mbalimbali, hivyo wizara yangu leo inatoa Sh212 milioni kwaajili ya malipo hayo," alisema Waziri Nyalandu.
Alisema silaha hizo zimekombolewa ikiwa sehemu ya kutekeleza maazimio ya Bunge na ahadi ya Serikali kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira.
Akizungumzia sababu za kuchelewa TRA, Nyalandu alisema kulikuwa na ubishi wa ama zilipaswa kulipiwa kodi au la, lakini mamlaka hiyo ilifafanua kuwa hayo ndiyo matakwa ya sheria, hivyo akaamua kutoa fedha hizo.
Alipoulizwa ni jinsi gani Serikali itadhibiti silaha hizo, Nyalandu alisema wizara yake inaandaa miikoya matumizi yake ikiwamo kufuatilia makabidhiano yake na askari wanaokabidhiwa.
"Kumbuka hizi si silaha za kwanza kuwa nazo, tunazo nyingine za AK47 na hizo zimetuwezesha kukamata silaha haramu zaidi ya 2,000 zinazotumiwa na majangili," alisema.
Silaha hizo zimepatikana ikiwa ni takriban wiki mbili tangu Rais Jakaya Kikwete abanwe na vyombo vya habari vya kimataifa akitakiwa kueleza mikakati iliyopo kupambana na ujangili ambao umeharibu sura ya Tanzania nje ya nchi.
Itakumbukwa kuwa miezi miwili iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alilazimika kupangua Baraza la Mawaziri na kuwatimua mawaziri wanne kutokana na vitendo vya kinyama vilivyobainishwa na Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
*MAJANGILI PAPA 40
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Waziri Nyalandu alisema majina ya majangili papa 40 ambayo Rais Kikwete alisema anayo, 'yatabandikwa' hivi karibuni.
"Serikali ina mkono mrefu sana, hatupendi mtu aache mke na watoto wake afungwe miaka 50. Kama ni majina tutayabandika, nimeshakubali, tutayabandika, ni kwamba tu sina hiyo orodha hapa," alisema.
Alisema, Serikali inawafahamu majangili hao kwa undani, wanapokunywa chai, wanapotembelea na shughuli zao za kila siku.
Alisema majina yao si siri kwani tayari wameshafunguliwa mashtakana wapo chini ya mfumo wa Mahakama na wamekamatwa na vidhibiti.
Hivi karibuni, Rais Kikwete alihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), alisema Serikali ina majina 40 ya majangili papa na mkuu wao yuko Arusha.
*SELOUS YAIMARISHWA
Katika hatua nyingine, Nyalandu alitangaza kuzipandisha hadhi kanda nane zilizopo katika Pori la Akiba la Selous ili ziweze kujitegemea kiutendaji kwa kuwekamkuu wa kila kanda.
Alisema pori hilo lina ukubwa unaokaribia hifadhi zote za Taifa chini ya Tanapa, jambo linalolifanyakuwa kubwa kimenejimenti na kiuendeshaji.
Pori la Selous lina kilomita za mraba 55,000 wakati mapori yote nchini kwa ukubwa wake ni kilomitaza mraba 57,000.
Katika kuweka mazingira ya uangalizi wa kina ya kupambana na ujangili aliiagiza Idara ya Wanyamapori kukamilisha mchakato wa kufungua akaunti maalumu za benki kwa kila kanda ili kuwawezesha wakuu wa kanda kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Chanzo:Mwananchi