MKE NA MUME WAZUA BALAA BUNGE LA KATIBA

Chama cha National League for Democracy (NLD) Zanzibar kimemtaka, Rais Jakaya Kikwete kufuta uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kupitia chama hicho kwa madai kuwa walioteuliwa katika chama hicho ni mtu na mkewe na kufanya uteuzi huo kukosa sura ya Muungano.

Tamko hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa NLD - Zanzibar, Khamis Haji Mussa katika taarifa aliyoisambaza kwa vyombo vya habari mjini hapa juzi, kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Dk Emmanuel Makaida amewasilisha majina mawili, la kwake na la mkewe, Modesta Ponera kwa ajili ya uteuzi.

Alisema NLD - Zanzibar kilianza kufuatilia taratibu za uwasilishaji wa barua tangu Desemba 27, mwaka jana kwa kumwandikia barua Katibu Mkuu Kiongozi wa SMZ baada ya kupokea maelekezo ya Ikulu ya Tanzania kwamba majina ya Zanzibar yatafanyiwa kazi visiwani na ya Bara yangepelekwa Ikulu Dar es Salaam.

Alisema kwa mujibu wa utaratibu huo, vyama vyote vyenye usajili wa kudumu vilitakiwa kila kimoja kutoa mtu mmoja kutoka Tanzania Bara na mwingine Zanzibar ili kuwa na sura ya kitaifa, lakini Dk Makaidi alikiuka utaratibu huo.

MAKAIDI AJITETEA

Akizungumzia tuhuma hizo, Dk Makaidi alikiri kuwa Ponela ni mke wake, lakini akasema ni mwanachama wa NLD, hivyo ana haki ya kuteuliwa.

Alisema alipeleka majina manne Ikulu na kwamba upande wa Zanzibar ulitakiwa kufanya hivyo kupitia Ikulu ya Zanzibar... "Walifanya uzembe, hawakupeleka majina ya wanachama wa NLD, matokeo yake nikapeleka majina manne,tukapata uwakilishi."

Alisema mkewe ni mwanachama wa NLD hivyo ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi yoyote kulingana na sifa zake...

"Wanalalamika nini hata chamatawala cha CCM, Rais Jakaya Kikwete ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) na Mkewe Salma pia ni mjumbewa Nec."

Alisema Ponela kuwa mkewe hakumfanyi akose haki zake za msingi na kwamba sifa zake na elimu ndivyo vilivyomfanya Rais amteue.

Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Florens Turuka alipoulizwa alisema Ikulu haina taarifa za suala hilo lakini wanaamini vyama vya siasa vilikaa na kupendekeza majina manne na kuyawasilisha Ikulu, ndipo Rais alipoteua wajumbe mawili kati yake.