SAKATA LA POSHO LAUNDIWA KAMATI

Sakata la posho kwa wajumbe wa bunge la katiba laundiwa kamati.

Sakata la posho na fedha za kujikimu kwa wajumbe wa bunge maalumu la katiba limechukua sura mpya baada ya mwenyekiti wa muda wa bunge maalum la katiba Mh. Pandu Amir Kificho kuteua majina ya wajumbe sita watakaounda kamati ya kujadili malalamiko ya wajumbe hao huku sheria na rasimu ya katiba zikiwasilishwa bungeni ambapo wajumbe wameonywa juu ya kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Hatua hiyo ya mwenyekiti wa bunge maalum la katiba imefikiwa baada ya uwepo wa mvutano kuhusu posho na fedha za kujikimu kwa wajumbe hao ulioibukia ndani ya ukumbi wa bunge wakati ambao waandishi wa habari walitolewa nje ya ukumbi huo katika kipindi ambacho wajumbe walikuwa wakikabidhiwa nakala za rasimu ya kanuni za bunge maalum kutokana na wajumbe wa Tanzania bara kupata taarifa kuwa wenzao wa baraza la wawakilishi, wanalipwa kiasi cha shilingi laki nne na ishirini elfu tofauti na wale wa bara wanaoolipwa kiasi cha shilingi laki tatu kwa siku.

Katika hatua nyingine mwanasheria mkuu wa serikali jaji Fredriki Werema amewasilisha sheria ya mabadiliko ya katiba na kuwatahadharisha wabunge kuhakikisha kuwa masuala ya uwepo wa jamhuri ya muungano, serikali, bunge na mahakama hayaguswi kwa namna yeyote ile na kuwataka wajumbe hao kujiepusha na rushwa wakati wa uchaguzi wa viongozi wa bunge hilo maalum.

Mara baada ya werema kuwasilisha sheria hiyo ya mabadiliko ya katiba wajumbe wakapata fursa ya kusimama kuomba ufafanuzi, kuuliza maswali ama kutoa michango yao kutokana na uelewa wao.