KENYA KUPELEKA MAJESHI SUDAN KUSINI

Kamati Kuu ya Usalama Nchini Kenya imependekeza kwa bunge liidhinishe nyongeza ya idadi ya wanajeshi wake wa kudumisha amani walioko nchini Sudan Kusini, chini ya kivuli cha Umoja wa Mataifa, kwa majeshi 310.

Kamati hiyo chini ya uenyekiti waRais Uhuru Kenyatta imesema imechukua hatua hiyo kufuatia ombi la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lililofanywa Desemba 24, mwaka jana.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa ikulu ya Nairobi usiku wa kuamkia leo, kamati hiyo ambayo imekutana kwa mara ya kwanza tangu Rais UhuruKenyatta kuanza utawala wake mwaka mmoja uliopita ilisema kuwa Kenya itawatoa wanajeshi wengine ili kufanya idadi ya wanajeshi wake walioko Sudan Kusini kufikia 1,000.

Taarifa hiyo ilieleza wazi kuwa wanajeshi wa Kenya wanaingia huko chini ya Umoja wa Kimataifa na wala sio kama taifa huru.

Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kuanza kati ya jeshila Sudan Kusini linalomuunga mkono Rais Salva Kiir na wanajeshi waasi wanaomuunga mkono makamu wa rais wa zamani Daktari Riek Machar, Uganda iliwatuma wanajeshi nchini humo kuunga mkono Rais Salva Kiir.

Katika taarifa hiyo kamati ya usalama nchini Kenya ilisema kuwa hali ya usalama nchini Sudan Kusini imeathiri Kenya.

Wakimbizi wengi wametorokea Kenya, taifa ambalo kwa hivi sasalinakabiliwa na matatizo yake mengi ya kiuslama kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi wa Somalia.

Miongoni mwa matatizo ya kiusalama yaliyotajwa katika taarifa hiyo ni mapigano kati ya makabila mbalimbali nchini Kenya na pia hatari ya mashambulizi ya kigaidi katika uwanja wake wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Mkutano huo wa usalama ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta ulisema usalama katika uwanja huo utaimarishwa kwa kuimarisha mitambo ya kuwapekua wasafiri wa kimataifa.

Nairobi ni kitovu kikubwa cha usafiri kwa watalii na wafanyabiashara katika eneo zima la ukanda wa mashariki na upembe wa Afrika.

Rais Uhuru Kenyatta hii leo atasafiri hadi mji Mkuu wa Sudan Kusini, Juba, kama hatua mojawapo ya viongozi wa eneo la Afrika Mashariki la kutafuta suluhu la mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini humo.


*OBAMA KUONDOA MAJESHI AFGHANISTAN

Rais Obama ameagiza makao makuu ya ulinzi nchini Marekani Pentagon kuandaa mipango ya kuwaondoa wanajeshi wake wote kutoka Afghanistan ifikapo mwisho wa mwaka huu iwapo hakutakuwepo maafikiano rasmi na Serikali ya Afghanistan.

Rais Obama alimpigia simu Rais Karzai wa Afghansitan juu ya mipango hiyo yake.

Rais Karzai amewaudhi Marekani kwa kukataa kata kata kutia sahihi muafaka ambao ungeruhusu baadhi ya wanajeshi kuendelea kukaa Afghanistan baada ya mud auliokubaliwa awali wa mwisho wamwaka huu wa 2014.

Mpango huo ambao tayari ulikuwa umekubaliwa na baadhi ya viongozi wa kikabila wa Afghanistan - unaandaa wajibu wawanajeshi wa NATO unaoshirikisha kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Afghanistan na kusaidia Serikali ya taifa hilo kukabiliana na wapiganaji wa Kitaliban.

Mkataba huo pia unawapa kinga ya kisheria wanajeshi wa Marekani walioko nchini Afghanistan.

Ikulu ya White House inasema kuwa hakuna uwezekano wa Karzai kutia sahihi mapatano hayo kabla ya kuondoka mamlakani Aprili mwaka huu.