Kiongozi wa mashtaka wa ICC Fatou Bensouda amekiri kuwa bado hana ushahidi wa kutosha kuwezesha kesi hiyo kuendelea.
Mawakili wanao mwakilisha Rais Kenyatta wanataka kesi hiyo kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi wa Kenya mwaka 2007 itupiliwe mbali.
Bensouda amesema kuwa bado kuna maswala yanayozua utata naambayo yanahitaji uchunguzi wa kina.
Mawakili wa Kenyatta wanatuhumu upande wa mashitaka kwa kusisitiza kutaka taarifa kuhusu akaunti ya benki ya Rais Kenyatta kuona ikiwa kuna pesa zozote zilizotolewa kwa lengo la kutumika wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuuwa mwaka 2007/08 Wakili wa waathiriwa mesisitizia mahakama kuwa kutupiliwa mbali kwa kesi kuwakosesha waathiriwa haki. Mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi katika siku chache zijazo.
ICC NA AFRIKA
Mataifa ya Afrika yamekuwa yakikosoa ICC kwa kulenga tu viongozi wa Afrika.
Kesi dhidi ya Kenyatta ni muhimukwa ICC ambayo imefanikiwa tu kumhukumu mtu mmoja huku nyingi ya kesi zinazofikishwa katika mahakama hiyo zikitupiliwa mbali kutokana na sababu nyingi tu tangu kubuniwa miaka 11 iliyopita.
Wadadisi wanasema kuwa huendakesi hiyo ikaleta msukosuko katika kanda ya Afrika Mashariki ikiwa viongozi wa mashitaka watasisitiza iendelee.
Rais Kenyatta alifikishwa ICC kutokana na tuhuma kuwa alikuwa mmoja wa washukiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya mwaka 2007/2008. Anakabiliwa na makosa ya mauaji na uhalifu mwingine dhidi ya binadamu.
Kadhalika Kenyatta alishitakiwa pamoja na makamu wake wa RaisWilliam Ruto kwa tuhuma sawa. Kesi dhidi ya Ruto inaendelea katika mahakama hiyo.
Mataifa ya Magharibi ambayo yanajitolea katika kuunga mkono ICC, pia yana wasiwasi kuhusu uhusiano wao na Kenya ambayo inaonekana kama mshirika mkubwa katika vita dhidi ya kundi la wanamgambo la Al Shabaab nchini Somalia.Watu 1,200 walipoteza maisha yao katika ghasia za uchaguzi mkuu mwaka 2007/08 huku maelfu wakilazimika kutoroka makwao. Wote wamekanusha mashitaka.
Viongozi wa mashitaka ICC wanasema kuwa Kenyatta aliongoza ghasia hizo lakini kesi dhidi yake imefanywa dhaifu kutokana na baadhi ya mashahidi kujiondoa katika kesi hiyo tangu kesi hiyo kuwasilishwa katika mahakama hiyo miaka minne iliyopita.
Kesi yenyewe ilitarajiwa kuanza Jumatano, lakini ikaahirishwa kwamara ya nne mwezi jana wakati ambapo wendesha mashitaka waliposema kuwa shahidi mwingine alijiondoa kwenye kesi huku wakiomba mahakama kuwapa muda zaidi kutafuta ushahidi.
Viongozi wa mashitaka wanasemakuwa mashahidi wengi wamehongwa au kutishwa kiasi cha kujiondoa katika kesi hiyo.