KAGAME KUKUTANA NA JK

MARAIS Jakaya Kikwete na Paul Kagame wa Rwanda, wamepanga kukutana mara kwa mara kujadili matatizo yanayoibuka na kuhatarisha amani baina ya nchi hizo.Pia Tanzania imechaguliwa kwa mara ya pili kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya utekelezaji ya mwaka ya Wizara yake.

"Kama itakavyokumbukwa, vyombovingi vya habari viliripoti kudorora kwa uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda. Baada ya mazungumzo kati ya Rais Kikwete na Rais Kagame jijini Kampala Septemba mwaka jana, hali ya uhusiano wetu iliboreka," alisema Membe. Hata hivyo, alisema hivi karibuni vyombo ya habari vya Rwanda ukiwamo mtandao wa "News of Rwanda" vilitoa taarifa za kuishutumu Tanzania na viongozi wake.

Pia alisema kumekuwa na taarifa za kuishutumu Tanzania kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani nchini Rwanda akiwamo Waziri Mkuu wa zamani wa Rwanda, Faustine Twagiramungu.

Membe alisema Serikali ya Tanzania ilishajibu shutuma hizo kwa kueleza kuwa Tanzania haisaidii vikundi vya waasi na haijawahi kufanya mazungumzo wala kukaribisha viongozi wa Upinzani wa Rwanda.

"Historia ya nchi yetu tangu uhuru inajulikana kuwa tumekuwa tukisisitiza amani Afrika na hivyo hatuna sababu ya kusaidia waasi kuchochea migogoro.

"Hivyo, tunaomba kuchukua nafasi hii kuonya wanaotaka kuchafua sifanzuri ya Tanzania kuacha mara moja. Aidha, tunaomba wanahabari kutoshabikia taarifa hizi za uzushi," alisisitiza.

Alisema tangu mwaka 1963 Tanzania imekuwa ikitumika kama makao makuu ya vyama vya kupigania uhuru na imekuwa ikipokea watu walioomba hifadhi na ushauri ambao huhifadhiwa na kusuluhishwa kisha hurejea nchini mwao.

"Kama tungekuwa na tunaingilia migogoro ya watu na kusaidia makundi fulani kwa historia ya nchihii, tungekuwa tunapigana vita na bara zima la Afrika," alisema.

Alisema Tanzania siku zote inataka uhusiano mzuri na jirani zake, lakini isiwe kupenda amani kwake kuwe sababu ya watu kutaka kuichafua.

Aidha, alisisitiza kuwa Tanzania haina mpango wala haifikirii kuanzisha mgogoro wa kivita na nchi yoyote ya jirani ikiwamo Rwanda, kwa kuwa nchi hizo ni kama ndugu kwa Watanzania na inapaswa kusaidiana.

Akizungumzia kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la UN, Membe alisema nchi hiyo imechukua nafasi hiyo kwa mara ya pili baada ya kushindakwa kura za nchi 40 kati ya 53.

Alisema sababu ya kuwania tena nafasi hiyo ni kutokana na heshimailiyojijengea kimataifa, hususan katika utatuzi wa migogoro ya kikanda kama ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Madagascar, lakini pia kuwa mstari wa mbele kuchangia vikosi vya kulinda amani kwenye maeneo yenye migogoro kama vile Darfur, DRC na Lebanon.

Sudan Kusini Kuhusu mgogoro unaoendelea Sudan Kusini, alisemaTanzania imeridhia ombi la Baraza la Usalama la UN kuitaka ipeleke vikosi vyake kujiunga na Jeshi la UN nchini humo na imeshaanza kujiandaa kupeleka bataliani moja.

Alisema Baraza liliiomba Tanzania kupeleka vikosi vyake nchini humo kutokana na sifa kubwa ambayo majeshi ya Tanzania yamejijengea nje ya nchi na kuheshimika.

"Lakini pia sisi tunataka kuanzisha mpango wa nchi za Afrika kushughulikia matatizo yao zenyewe na si kutegemea majeshi ya nchi za Magharibi," alisema.

Ujangili Kuhusu mkutano ulioandaliwa na Mtoto wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, David Cameron wa kuzuia biashara ya pembe za ndovu, Membe, alisema Rais Kikwete atayapitia maagizo yaliyotolewa katika mkutano huo ikiwemo kutouza pembe za ndovu zilizokamatwa na kuhifadhiwa hapanchini na badala yake kuziteketeza.

"Kama mnakumbuka, tuliomba ruhusa ya kuuza pembe hizi za ndovu tulizokamata kutoka kwa majangili ili kupata fedha za kuwapeleka kwenye mafunzo askari wa Wanyamapori, kununulia vifaa na magari ya ulinzi katika hifadhi zetu, lakini katika mkutano huo, Uingereza ilikataa kuziuza bali tuziteketeze," alisema.

Alisema iwapo Rais ataridhia kuziteketeza, inabidi suala la malipo ya fidia lizungumzwe ili kupatikana kwa fedha kwa ajili ya maandalizi mazuri ya kukabiliana na majangili hao.

Uraia Kuhusu suala la uraia wa nchimbili, alisema Wizara yake imeandaa taarifa ya kuwasilisha kwenye Bunge Maalumu la Katiba inayotaka suala hilo liingizwe na kuruhusiwa nchini ili kusaidia Watanzania walioko nje nao waweze kushiriki shughuli za kiuchumi nchini.

"Tumeona hatuwapatii haki Watanzania walio nje wenye uraia wa nchi nyingine kwa kuwanyang'anya uraia wa Tanzania, wakati nchini kuna sheria inayoruhusu raia wa nje aliyeishi nchini kwa miaka 10 kupewa uraia akiomba," alisema.