MKURUGENZI WANYAMAPORI ATIMULIWA

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amemuondoa katika nafasi yake Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa na kumteua Paul Sarakikya kukaimu nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa yake aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Nyalandu alisema amechukua hatua hiyo kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa kazi wa idara hiyo katika mapambano dhidi ya ujangili, yanayoendelea nchini.

"Aidha hatua hii ni utekelezaji wa Azimio la Bunge lililotolewa Desemba 22, mwaka jana lililotaka Mkurugenzi wa Wanyamapori kuwajibishwa kutokana na tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa haki za binadamu katika Operesheni Tokomeza," alisema.

Alisema pia amemuondoa Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Jafari Kidegesho na kumteua Dk Charles Mulokozi kuchukua nafasi hiyo.

Katika mabadiliko hayo, Nyalandu pia alimteua Julius Kibebe kuwa Mkurugenzi Msaidizi Uzuiaji- Ujangili huku Mkurugenzi Msaidizi Uzuiaji-Ujangili na Takwimu, Nebbo Mwina akiendelea kushika nafasi hiyo.

Alisema Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji wa Wanyamapori, Herman Keiraryo naye anaendelea kushikilia wadhifa huo.