MVUA YAUWA NA KUEZUWA NYUMBA

Nyumba 62 zilizopo katika Vijiji vya Wilaya ya Kilindi, zimeezuliwa na nyingine kubomoka kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga.

Maafa hayo yamesababisha mtoto mmoja kufa kwa kuangukiwa na nyumba, huku zaidi ya wanavijiji 110 kukosa mahala pa kuishi.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Selemani Liwowa ni kuwa nyumba hizo zimeezuliwa usiku wa kuamkia Ijumaa wiki iliyopita baada ya kunyesha mvua iliyoambatana na upepo.

Mvua kubwa ilinyesha katika vijiji mbalimbali vya wilayani hapa na kusababisha madhara hayo.

Akithibitisha tukio hilo, Liwowa alivitaja vijiji vilivyokumbwa na maafa hayo kuwa ni Songe, ambako mtoto mmoja amekufa kwa kuangukiwa na ukuta.

Vijiji vingine ni Kwasetemba, ambako nyumba 16 zimeanguka naGitu zilikobomoka na kuezuliwa ni nyumba 42.

Alisema ya maafa hayo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Kilindi iliweza kutembelea kwa lengo la kujionea athari, ambapo hatua inayofuata ni kutuma wataalamu kutathimini athari na mahitaji kwa waathirika.