MAJAMBAZI WAVAMIA SHULE YA SEKONDARI, WAUWA MWANAFUNZI MMOJA

Majambazi nchini Kenya wamemuua mwanafunzi mmoja wa shule ya upili na kuwajeruhi wengine wengi katika uvamizi waliofanya dhidi ya shule ya mabweni ya St Charles usiku wa kumakia leo.

Wanafunzi wa shule hiyo iliyo viungani mwa Nairobi,walisimulia ambavyo majambazi waliwashambulia usiku wa manane wakiwa wamelala katika mabweni yao na kusababisha kifo cha mmoja wao.

Wanafunzi walionusurika walisema majambazi hao ambao idadi yao inakadiriwa kuwa hamsini , walivunja madirisha na milango na kisha kuingia katika mabweni yao.Waliwachapa wanafunzi kwa mijeledi na kuwapiga mawe na kisha kuwashuturisha kutoroka.

Baada ya uvamizi huo walitoka nje na kuharibu magari ya walimu yaliyokuwa yameegeshwa nje pamoja na mabasi ya shule. Ni nadra kusikia uvamizi kama huu dhidi ya shule.

Mkurugenzi mkuu wa shule hiyo bwana Charles Niyamote aliambia BBC kuwa nia ya wavamizi haijulikani ingawa alidokeza kwamba huenda ni wivu uliowachochea majambazi hao kutenda uhalifu huo.

Hata hivyo tetesi zinasema kuwa huenda ni mzozo wa ardhi uliosababisha uhalifu huo.

Kwa sasa shule hiyo imefungwa kwa muda wa wiki moja wakati polisi wakiendelea na uchunguzi wa kina.

Visa vya ukosefu wa usalama vimeongezeka katika mji wa Nairobina viunga vyake katika siku za hivi karibuni na pia sio jambo la kawaidakwa wanafunzi kuvamiwa shuleni nchini Kenya.