GAVANA WA BENKI KUU ATIMULIWA KAZI NA RAIS

Gavana wa benki kuu ya Nigeria, Lamido Sanusi amesimamishwa kazi kwa muda akisubiri matokeo ya uchunguzi wa kile kinachosemekana kuwa makosa makubwa katika rekodi za benki.

Bwana Sanusi alizua hisia nchini Nigeria aliposema kuwa Dola Bilioni 20 za mapato yaliyotokanana mafuta hazijulikani ziliko.

Shirika la mafuta la serikali, limekanusha madai kuwa halijawasilisha rekodi zake kuhusu lilivyotumia pesa hizo likisema kuwa madai hayo hayana msingi.

Bwana Sanusi anaheshimika sana nchini Nigeria hasa baada ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya benki tangu kuteuliwa kama gavana mwaka 2009 Alitajwa kuwa gavana bora zaidi wa beni kuu mwaka 2010 na jarida la Banker magazine.

Nigeria ni moja ya nchi zenye kuzalisha mafuta kwa wingi duniani lakini sekta hiyo imekuwa ikikumbwa na madai ya wizi na ufisadi.

Mnamo mwezi Februari, bwana Sanusi aliambia kamati ya Baraza la Senate kuwa kati ya Dola Bilioni 67 za kimarekani thamani ya kiwango cha mafuta kilichouzwa kati ya mwezi Januarimwaka 2012 na Julai 2013, dola bilioni 20 bado hazijajulikana ziliko.

Shirika la mafuta la serikali lilisema kuwa madai hayo sio ya kweli na kwamba hayana msingi.

Bwana Sanusi anahudhuria mkutano wa kikanda wa wakuu wa benki kuu nchini Niger.

Nafasi yake itachukuliwa na naibu wake Sarah Alade, aliyeandamana naye kwenye mkutano huo.

Rais Jonathan alimuomba Sanusi kujiuzulu mwezi Disemba lakini akakataa.

Rais hana mamlaka ya kumfuta kazi gavana wa benki kuu. Ni bunge pekee linaloweza kufanya hivyo.

Muda wake unapaswa kukamilika mwezi Juni lakini duru zinasema kuwa uamuzi wa kumwachisha kazi kwa muda ni muhimu sana.

Taarifa ya Rais ilisema kuwa Sanusi anaachishwa kazi kwa sababu ya kuvunja sheria za benki kuu.