BENKI YA DUNIA YABANA MSAADA KWA UGANDA

Benki ya dunia imebana msaada wa dola milioni 90 kwa Uganda , siku chache tu baada ya Rais Yoweri Museveni kuizinisha sheria mpya dhidi ya mapenzi ya jinsia moja.

Benki hiyo imesema kuwa inataka kufanya tathmini yake kuhakikisha kuwa malengo yake ya maendeleo nchini Uganda katika sekta ya afya, ambayo msaada huo ulikuwa unanuiwa, hayata athirika.

Sheria iliyoidhinishwa na Rais Yoweri Museveni, ilitiwa saini Jumatatu na inatoa adhabu kali kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Wafadhili wengine tayari wameanza kusitisha misaada Uganda.

Wahisani kama Denmarkna Norway wamesema kuwa wataanza kufadhili mashirika moja kwa moja badala ya serikali.

Aslimia 20% ya bajeti ya Uganda inategemea michango ya wafadhili.

Mpaka sasa nchi tatu za Ulaya zimeamua kukata misaada yao kwa mamilioni ya dola.

Wizara ya fedha ya Uganda imesema inasubiri mawasiliano rasmi ya nchi husika, na iko tayari kukabiliana na athari za hatua hiyo.

Hadi kufikia sasa Waziri wa FedhaWa Sweden, akiwa mjini Kampala, alisema waekezaji kutoka nchi yake watakuwa na wakati mgumu kuweka pesa zao nchini Uganda kwa sababu watakuwa na hofu kuwa sheria yoyote inaweza kupitishwa kuwadhulumu watu.

Jana serikali ya Uholanzi ilisema itazuia kwa muda misaada kwa Serikali ya Uganda.

Norway na Denmark pia zimetangaza kupunguza au kusimamisha kwa muda misaada yake kwa Uganda.