MAKADA WALIOHOJIWA WAPIGWA ADHABU

MAKADA sita wa CCM waliohojiwa hivi karibuni na Kamati Ndogo ya Maadili ya Chama hicho wamepewa onyo kali linaloendana na kuwekwa chini ya uangalizi kwa mwaka mmoja.

Waliokumbwa na adhabu hiyo ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Steven Wasira.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na Waziri wa zamani wa Nishati, William Ngeleja. Hatua hiyo imechukuliwa dhidi yao baada ya kuthibitika kuwa walianza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais wa nchni mwakani kabla ya wakati.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya Kamati Kuu ya Chama hicho, kuhusu wanachama hao waliohojiwa kuanzia Februari 13 hadi 18.Alisema baada ya kuwahoji walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea uraiskabla ya wakati, jambo ambalo ni kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili ya Chama hicho.

Pia walithibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo hivyo ndani ya jamii."Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa wote adhabu kali na kutaka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili naiwapo wataendelea navyo, chama kitawachukulia hatua zaidi," alisema Nnauye.

Alitoa tafsiri ya adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za chama hicho,kuwa:

"Mwanachama aliyepewa adhabu ya onyo kali atakuwa katika uchunguzi kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia jitihada zake za kujirekebisha."

Alisema akiwa katika kifungo hicho mhusika atakuwa amepoteza sifa za kugombea nafasi yoyote sawa na mtu aliye na kifungo cha nje ambacho kinamtaka asifanye kosa lolote. Alisema Kamati Kuu iliitaka pia Kamati Ndogo ya Udhibiti kuchunguza na kuwachukulia hatua wote waliohusika kwa namna moja au nyingine, mawakala na wapambe kufanyika kwa vitendo vilivyovunja kanuni za chama.

"Aidha, Kamati Kuu imewaonya viongozi na watendaji wa chama nakuwataka kujiepusha na matendo ya wanawania urais yanayovunja nakukiuka maadili ya chama na wametakiwa kuzingatia kanuni na taratibu za chama," alisema.

Akizungumzia hatima ya wanachama hao alisema itategemea na tabia zao na ikiwa vikao husika vitaridhika ndipo hatima yao itajulikana.

Kauli ya JK Wakati huo huo, Nnauye alisema Rais Jakaya Kikwete hatafuta kauli ya kutaka wanachama wa chama hicho kuacha unyonge katika vurugu zinazofanywa na vyama vingine katika uchaguzi mbalimbali bali ataongeza nguvu.

Pia alisema Chadema haina adabu kwa kumpa Rais siku tatu aombe radhi kwani alitoa kauli hiyo kutokana na matendo inayofanya.

Alidai katika uchaguzi uliopita wa madiwani, viongozi na wanachama wa Chadema walifanya vitendo vyakinyama dhidi ya wana CCM wakitumia silaha kama mapanga, visu, bisibisi na marungu.

Nape alionya kutohamasisha mapambano katika uchaguzi mdogo, kwani vitendo vilivyofanyika katika uchaguzi wa udiwani pekee vinatisha na kama ndivyo itakuwaje katika uchaguzi mkuu. Alisisitiza kuwa CCM inapeleka vijana wake Kalenga ili kujilinda na matendo kama hayo.

"Hatujawahi kuwa na makundi kwa ajili ya kupiga watu bali kujilinda na watu wetu na wapigakura kwani Chadema hawataki siasa za kistaarabu," alisema.

Walipohojiwa Walipohojiwa wiki iliyopita, makada hao sita kila mmoja alitoka na kauli yake ambapo baadhi walikana kuwekwa 'kitimoto' wakidai walikuwa wakitoaushauri, huku mmoja 'akifunguka' na kueleza dhahiri kilichojiri ndani ya kikao hicho ambacho kilikuwa kikifanyika si chini ya saa moja na nusu.

Lowassa aliyekuwa wa kwanza kuhojiwa, alisema kilichoongewa ni masuala ya kujenga chama.

"Tumeshauriana na kukubaliana vizuri tu ili kukisaidia chama kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015," alisema. Kuhusu madai kwamba anatajwa kushiriki kuvuruga chama kwa kuanzisha makundi, alisema kitu kama hicho hakikuzungumzwa.

"Sijibu lawama, kwa vile hakikuwa kikao cha lawama, kilikuwa cha mazungumzo na ndani ya kikao hakukuzugumzwa makundi," alisema Lowassa Sumaye Sumaye akiwa wa pili kuhojiwa, alisema;

"Itabidi muwasubiri wakubwa," na kufafanua kwamba baada ya Kamati hiyo kutoa majibu ya kilichojadiliwa, atakuwa na la kusema, lakini kwa siku hiyo hakuwa na cha kuongea.

Ngeleja, baada ya kutoka, alisema kikao kilikuwa kikizungumzia mambo ya kichama zaidi na kwamba ndani ya CCM, wanaongozwa na kanuni na wenye nia ya kugombea muda bado haujafika na si jambo la ajabu chama kuita watu wake kuwahoji.

"Binafsi sijatangaza nia ya kugombea urais… kama kuna ugomvi mimi siko kwenye ugomvi huo," alisema Ngeleja. Makamba Januari alifuata baada ya Ngeleja na kusema hakukuwa na mashitakabali ushauri kuhusu namna ya kupata viongozi ili kuimarisha chama badala ya kukigawa hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

"Hakukuwa na habari ya mashitaka bali kutoa ushauri na kukumbushana misingi ya namna ya kupata uongozi na kuimarisha chama badala ya kukigawa," alisema.

Wasira Wassira aliyefuata baada ya Januari, na kusema hajawahi kutangaza nia ya kugombea urais na wala si dhambi mtu kutamani kuwa Rais wa Nchi.

Alisema hakuitiwa tuhuma ila waandishi wa habari walifanya mkutano uwe wa tuhuma, lakini walizungumzia mustakabali wa kuelekea uchaguzi mkuu mwakani. Alisema magazeti mengi yaliripoti kuwa wanaitwa kwa tuhuma ya kutangaza nia kabla ya wakati.

"Sijawahi kutangaza kugombea urais…kwani ni kosa kutangaza kugombea urais?" Alihoji Wasira nakuongeza: "Kuna barua na magazeti ambayo yanatofautiana juu ya kuitwa Dodoma, andikeni ukweli mimi ni mjumbe wa KamatiKuu siwezi kuvuruga chama.

"Membe Membe akiwa wa mwisho kuhojiwa, alisema pamoja na baadhi ya wenzake kudai hakukuwana mashitaka, waliitwa kuhojiwa.

"Kamati yetu ya Maadili imejipanga vizuri, na msidanganyike, wanauliza maswali mazito, maswali magumu ama unayoyafanya wewe au mashabiki. Lakini yote yanalenga katika kukiimarisha chama, katika kuimarisha ushindi kwa mwaka 2015 na kuimarisha maadili. Yale ni mambo mazito," alisema Membe na kuongeza:

"Makubwa matatu ambayo Kamati ya Maadili iliuliza, kubwa kabisa ni uzukaji ghafla wa makundi ambayo yanazaliwa kila watu wanapodhani fulani anafaa kuwa kiongozi.

Tunafanyaje kukifanya chama chetu kiwe na kundi moja litakalokwenda mwakani kwenye ushindi."

Lakini la pili, pia ni suala zima la fedha kama msingi wa ushindi. Inatokeaje watu wanatumia mamilioni, mabilioni ya fedha kujinufaisha na kujiandaa kwenda kwenye uchaguzi.

"Lakini tatu ni vyombo vya habari; ninyi waandishi wa habari, mnalishwa vitu gani, mmemeza nini vichwani mwenu mpaka mwone kinachosemwa na fulani ni cha maana hadi kitoke katika magazeti na kingine kikisemwa na fulani, hata kikiwa cha maana kisitoke magazetini, mmemeza mdudu gani?" Alihoji Membe.