Bwana Yanukovych amekataa kusalimu amri licha ya bunge hapo awali kupiga kura ya kumuondoa ofisini.
Akizungumza katika runinga moja katika mji wa Kharkiv ,bwana Yanukovych ameelezea vitendo vinavyofanyika dhidi ya serikali yake kama vya mapinduzi.
Magavana wa majimbo ya mashariki mwa Ukrain wamefanya mkutano katika mji wa Kharkiv, uliohudhuriwa na maafisa wa Urusi ili kuzungumzia kuhusu udhibiti haramu wa mji mkuu wa kiev.
Mwandishi wa BBC anasema kuwa hiyo ni ishara tosha ya kutokea kwa mgawanyiko nchini humo mbali na kuongezeka.
Wakati huohuo aliyekuwa waziri mkuu wa Ukrain Yulia Tymoshenko ambaye amewachiliwa huru na bunge baada ya kuhudmia kifungo cha miaka miwili jela amepokelewa na hisia tofauti alipokuwa akiwahutubia maelfu ya waandamanaji katika medani ya Uhuru katikati ya mji mkuu wa Kiev.
Akiwa ameketi katika kiti cha magurudumo, amewaambia waandamanaji kwamba wanasiasa nchini humo hawana thamani ya 'tone la damu yao' iliomwagika wakati wa maandamano hayo.
Lakini mwandishi wa habari wa BBC amesema kuwa watu wengi katika kongamano hilo waliondoka wakati bi Tymoshenko alipoanza kuhutubia umati huo, wakisema kuwa hawakilishi upinzani.
Wengi waliohojiwa wameiambia BBC kwamba hawamtaka kuwa rais mpya.