KESI DHIDI YA BOSCO NTAGANDA KUANZA ICC LEO

Kesi dhidi ya aliyekuwa kiongozi wa waasi nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Bosco Ntaganda, inatarajiwa kuanza hii leo katika mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Mahakama hiyo inatarajiwa kuamua ikiwa Bosco Ntaganda atafunguliwa mashtaka ya mauaji, ubakaji, utumwa wa ngono na kuwasajili watoto jeshi.

Mshukiwa huyo ambaye pia anafahamika kama ''The Terminator'' ni mwanzilishi kwa kundi la waasi la M23, ambalo lilishindwa na utawala wa Kinshasa mwaka uliopita, baada ya miezi kumi na nane na mapigano makali, katika eneo la Kivu ya Kaskazini, Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Lakini atakapofika mbele ya mahakama hiyo, Ntaganda atafunguliwa mashtaka kumi na tatu ya uhalifu wa kivita na mengine matano ya ukatili wa kibinadam, uhalifu uliotekelezwa zaidi ya miaka kumi iliyopita wakati alipokuwa mbabe wa kivita katika eneo la Ituri, Kaskazini mwa Congo.


*ZAIDI YA WATU 800 WALIUWAWA

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Fatouh Bensouda, amesema kuwa takriban watu mia nane waliuawa na wapiganaji wa Patriotic Foces for Liberation of Congo, FPLC, walioongozwa na Bwana Ntaganda.

Wengi wa wapiganaji wake walitoka kabila la Hema ambao walikuwa wakipambana na wapiganaji wa wa Lendu, kuthibiti maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizowasilishwa na Bensouda katika mahakama hiyo, Ntaganda aliongoza na kuidhinisha mashambulio kadhaa dhidi ya watu wa kabila la Lendu.

''Wanjaeshi wa Ntaganda walishambulia vijiji kadhaa kwa kutumia silaha nzito nzito na kuwafukuza watu, huku wakifanyamsako wa nyumba hadi nyumbana pia katika misitu iliyokuwa katika eneo hilo'' Alisema Bensouda.

Kiongozi huyo wa zamani wa waasi anatuhumiwa kuharibu mali ya raia kwa kuteketeza makaazi yao baada ya kupora mali.


*ATUHUMIWA KUSAJILI WATOTO JESHINI

Ripoti zinasema Ntaganda alizuru kambi kadhaa ambako watoto walio na chini ya umri wa miaka kumi na mitano walipewa mafunzo ya kijeshi na kuwa alifanya mashambulio pamoja nao.


Katika kikao chake cha kwanza katika mahakama hiyo mwezi Machi mwaka uliopita, Ntaganda aliwaambia majaji hao wa ICC kuwa ''Nimefahamishwa kuhusu mashtaka ya uhalifu yanayonikabili na kuwa anakiri kuwa hana hatia'' Majaji wa mahakama hiyo ya ICC wana muda wa wiki mbili kuamua ikiwa kesi dhidi ya Bwana Ntaganda itaendelea au la.

Mshukiwa mwingine ambaye alifunguliwa mashtaka kwa pamoja na Ntaganda alihukumiwa kifungo cha miaka kumi na minne gerezani.

Ntaganda ni mshukiwa wa kwanza ambaye alijisalimisha kwa mahakama ya ICC, baada ya kujisalimisha kwa ubalozi wa Marekani mjini Kigali miezi kumi na moja iliyopita na kuomba awasilishwe kwa mahakama ya ICC.


*NTAGANDA ALIJISALIMISHA KWA NIA GANI?

Wachanganuzi wanasema kuwa Ntaganda alihofia maisha yake kama mtoro kutoka kwa viongozi wengine hasimu wa M23 lakini hadi sasa dhamira ya kujisalimisha kwake haijajulikana.

Mahakama ya ICC ilitoa vibali vyakukamatwa kwa Ntaganda mwakawa 2006 na nyingine iliyokuwa na mashtaka zaidi mwaka wa 2012.

Ntaganda ambaye alizaliwa mwaka wa 1973, ni Muafrika wa tano ambaye anazuiliwa na mahakama hiyo ya Kimataifa ya Jinai.

Kiongozi huyo wa waasi alikwea kukamatwa wakati vibali hivyo vilitolewa kwa kuwa alikuwa afisa mwandamizi jeshini.

Mwaka wa 2006, aliteuliwa kiongozi wa CNDP, kundi lingine la waasi la watu wa kabila la Watutsi lililoongozwa na Laurent Nkunda.


Mapigano nchini Congo yalimalizika kufuatia mkataba wa amani ulioidhinisha waasi hao kuteuliwa kujiunga na jeshi la serikali. Ntaganda naye akateuliwa kuwa generali katika jeshi la serikali na mara tu akaanza kuunda kikosi chake ndani ya serikali.

Kwa mara nyingine tena alifufua mitandao yake na mwaka wa 2012 aliunda kundi la M23, wakati rais Joseph Kabila alipoonyesha ishara kuwa yuko tayari kutekeleza agizo la mahakama ya ICC ya kumkamata na kumuwasisha mbele ya mahakama hiyo.

Umoja wa Mataifa umeishutumu Rwanda kwa kumfadhili Ntagandana kundi lake la M23, madai ambayo yamepingwa vikali na utawala wa rais Paul Kagame.