WABUNGE WAKATAA POSHO YA 300,000 KWA SIKU

WAKATI mjadala wa kihistoria wa kuunda Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukiwa katika hatua ya kupata kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, baadhi ya wajumbe wameamua kuelekeza nguvu kudai posho nono.

Wajumbe hao wanapinga posho ya sasa ya Sh 300,000 kwa siku, ambayo kwa wananchi wa kawaida inaonekana ni kubwa, lakini vielelezo vyao ni taarifa, kwamba wajumbe ambao wanatoka Baraza la Wawakilishi, wanalipwa zaidi ya hapo.

Mbali na hoja hiyo ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ambayo sasa wajumbe ambao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wanafikiria kumbana Spika Anne Makinda, ili nao waongezwe posho kama wenzao wa Zanzibar, hoja nyingine imetajwa kuwa ni hadhi yawabunge kwamba haifanani na Sh 300,000.

Aliyeanzisha hoja hiyo jana ni Richard Ndassa, Mbunge wa Sumve,ambaye mbali na kutaka nyongeza ya posho, alipinga utaratibu wa kusaini asubuhi na jioni kwa ajili ya posho zinazotolewa 'rejareja', akipendekeza waaminiwe na walipwe fedha nyingi kwa mkupuo.

Mjumbe mwingine, Suleiman Nchambi, alimwunga mkono Ndassa, lakini akahoji iweje wajumbe wa Tume ya Kurekebisha Katiba walipwe posho kubwa nao walipwe kidogo.

Mezani kwa Serikali Kutokana na hoja hizo, Mwenyekiti wa muda wa Bunge, Pandu Ameir Kificho, alisema suala hilo linachukuliwa kwa umuhimu na watazungumza na Serikali liamuliwe baadaye.

"Kuhusu masuala ya posho, kama nilivyosema tunalichukua ili tuangalie uwezekano wa kuzungumza na Serikali, hili tutaamua hapo baadaye," alisema Kificho.

Tume Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, Ndassa alisema wajumbe wa Tume walikuwa wakilipwa Sh 500,000 kwasiku huku madereva wakilipwa Sh 220,000.

"Mimi ninayehangaika kuanzia asubuhi na mimi nalipwa Sh 220,000? Mimi mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na dereva wa Tume ni sawa?" Alihoji Ndassa.

Katika Sh 300,000 kwa siku, Sh 80,000 ndiyo posho ya kujikimu ambayo wajumbe wa Bunge la Katiba watapewa kila siku, iwe amefanya kazi au la, na Sh 220,000 ni posho ya kazi, ambayo itatolewa kwa waliofanya kazi tu.

Hadhi ya Mbunge "Mimi kwenye hizi laki tatu (Sh 300,000) zangu zote, ni pamoja na dereva wangu, simu, chakula, mafuta, lakini pia unamtaka mbunge eti lazima asaini kwanza!" Alionesha mshangao.

Bila kupendekeza kiwango cha kulipwa, Ndassa alitoa mchanganuo wa matumizi ya mbunge, akisema hoteli ya hadhi yake ni Sh 70,000 kwa usiku mmoja.

Mbali na gharama hiyo ya malazi, alisema gharama za chakula, mafuta ya gari, dereva na msaada atakaotakiwa kutoa kwa watu mbalimbali Sh 80,000 haitoshi.

"Hoja yangu ya msingi, ni kwamba Serikali ijaribu kuangalia suala hili kwa upana, tukiliacha hivi hivi linaweza kuleta tatizo," alisema Ndassa.

Kususa Ndassa alisema wabunge wengine ni wafanyabiashara ambao hawawezi kukubali kukaa bungeni kwa muda wote wakilipwa posho ya Sh 300,000.

Alipohojiwa anatarajia mtazamo gani kutoka kwa wananchi wanaoishikwa kipato cha chini ya dola moja kwa siku (Sh 1,600), huku yeye akikataa Sh 300,000 kwa siku, Ndassa alisema:

"Ukiweka matarajioya jamii itasemaje, huwezi kufanya kazi. Maswali kama hayo huwezi kuyakwepa, binadamu hamwezi kulingana nyote duniani, hata vidole viko tofauti."

Nchambi alisema kwa upande wao, wabunge hawana tatizo isipokuwa anatetea wajumbe wengine ambao hawalipwi kiinua mgongo wala mshahara.

"Mbunge anatakiwa alale kwenye hoteli ya angalau Sh 70,000. Hata wananchi wanatakiwa waelewe kwamba wabunge wamekuja kufanyia kazi Katiba ambayo ndiyo msingi wao," alisema Nchambi.

Ubaguzi Suala lingine lililoibuliwa na Ndassa nje ya ukumbi, ni kuhusu tofauti ya kiasi cha posho kwa alichosema wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wameongezwa Zanzibar wakati wengine wakipokea Sh 300,000.

Bila kutaja kiasi kilichoongezwa, Ndassa alisema:

"Lakini wenzetu Wazanzibari wameongezwa na Baraza la Wawakilishi, wote ni wajumbe wa Bunge hilohilo… lazima kutakuwa na mgawanyiko. Na sisi tukisema hawa wabunge wamekwenda kwao wameongezwa na sisi tumwambie Makinda atuongeze, hawa makundi maalumu watakwenda kuongezwa wapi? "Kwa kufanya hivyo umeshaweka mgawanyiko inatakiwa tuwe kitu kimoja, kama ni Sh 20 wote tupeweSh 20, kama ni Sh 800 wote tuwe sawa," alisema Ndassa.

Mwandishi wa habari hizi hakufanikiwa kumpata Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad kufafanua hilo kutokana na kuwa kwenye kikao.

Lakini taarifa kutoka kwa baadhi ya watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), zilithibitisha kwamba wawakilishi waliomba waongezwe Sh 500,000 lakini hawakupewa zote; wamepewa chini ya hapo.

"Si kweli (hawapokei Sh 420,000) lakini waliomba Sh 500,000 ila hawakupewa hizo, wamepewa chini ya hapo," alisema mtoa habari ambaye hakusema ni kiasi walichoongezwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Utaratibu Kwa mujibu wa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, wabunge hao wameshapewa posho ya kujikimu ya Sh 80,000 kwa siku kuanzia Februari 16 hadi 28.

Aliongeza kuwa posho maalumu ya kazi ya Sh 220,000 kwa siku, ambayo hupigiwa hesabu kutokana na ushiriki wa mjumbe kusaini mahudhurio kila siku asubuhi na jioni, itakuwa ikiingizwa kwenye akaunti za wajumbe kila baada ya wiki moja ya kazi.


Chanzo: Habari leo