KENYA KUTOTEKELEZA MATAKWA YA ICC

Mwanasheria mkuu wa Kenya Profesa Githu Muigai ameiambia mahakama ya kimataifa ya ICC kwamba serikali ya Kenya haiwezi kutekeleza matakwa ya kiongozi wa mashitaka katika mahakama hiyo ya kuwashurutisha mashahidi waliojiondoa kutoka kesi inayomkabili Rais Uhuru Kenyatta kwenda kutoa ushahidi.

Pia amesema kuwa hawawezi kuagiza kutolewa kwa nyaraka za Benki za Rais Kenyatta za wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi miaka sita iliyopita.

Profesa Githu Muigai amekuwa mbele ya mahakama ya ICC kujibu madai ya upande wa mashtaka kwamba serikali ya Kenya imekuwa ikiweka vizingiti kwenye kesi dhidi ya Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto.

Kiongozi wa mashitaka Fatou Bensouda alitaka serikali ya Kenya iwasilishe stakabadhi za Benki za Rais Kenyatta za wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi.

Pia alitaka serikali iwalazimishe mashahidi saba waliojiondoa kutoka kesi hiyo kwenda ICC kutoa ushahidi, akidai walijiondoakutokana na shinikizo za serikali.

Lakini Bwana Muigai ameiambia mahakama kwamba mkataba wa Roma uliobuni mahakama ya ICC hauruhusu mashahidi kushurutishwa kutoa ushahidi.

Kuhusu kutolewa nyaraka za Benki za rais Uhuru Kenyatta, Bwana Muigai amesema ombi hilo lilitakiwa kutoka kwa majaji wanaosikiza kesi na wala sio kiongozi wa mashitaka.

Lakini pia amesema sio jukumu lake kuagiza kutolewa kwa stakabadhi hizo, bali ni mchakato wa mahakama, ambayo inaweza kuridhia ombi hilo, au kulikataa kama idara huria.

Mawakili wa Bwana Kenyatta wanataka kesi hiyo itupiliwe mbali, huku kiongozi wa mashitaka Bi Bensouda akitaka iahirishwe kumpa muda kusubiri nyaraka hizo ambazo anasema zitampa ushahidi zaidi wa kujenga hoja. Kikao kitaendelea hapo kesho.