AUWA MTOTO KWA KUMCHINJA NAE AUWAWA KWA MAWE

Watu wawili wamefariki dunia katika tukio lililokuwa na mwendelezo, mmoja akimchinja mtoto na yeye kuuawa kwa kupigwa mawe na wananchi wenye hasira.

Polisi walithibitisha mauaji hayo ya kutisha na kueleza kuwa yalitokea juzi saa 12 jioni maeneo ya Mbagala Charambe Foma, jijini Dares Salaam, ambapo katika tukio la kwanza Mohamed Said (36), alimkamata Jamal Salum (12) aliyedaiwa kuwa mwanafunzi wake na kumchinja kama kuku.

Habari zinaeleza kuwa Said akiwa nyumbani kwake alimkamata Jamal ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Nzasa na kumlaza chini, kisha akamchinja.

Hali hiyo inaelezwa kuibua hasira za wananchi wenye hasira na kuvamia nyumbani kwa Said na kumpiga mawe hadi naye kupoteza uhai wake.

Mkuu wa Upelelezi, Wilaya ya Kipolisi Mbagala, ASP Walelo, alieleza kuwa siku ya tukio (Juzi), Jamal alikuwa na mwenzake Ramadhani Salum (11) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne, Shule ya Msingi Kichechem aliyemsindikiza Jamal katika nyumba ya Said ambapo mjomba wake amepanga na walipokuwa wakitoka wakakutana na Said, ambaye alimshika Jamal, akamlaza chini na kumchinja kwa kutenganisha kichwa na kiwiliwili.

"Wakati akimchinja, Ramadhani akakimbia kutoa taarifa kwa watu waliokuwa karibu, walipofika walikuta tayari Salum ameshachinjwa," alisema Walelo nakuongeza:

"Baada ya hapo, wananchi wenye hasira walivunja mlango wa nyumba ya Said na kumkuta akiwa ameshika kisu alichofanyia mauaji na kumpiga hadi kupoteza maisha."

Alifafanua kuwa Said, anafanya kazi katika Shule ya Al-nur-al iliyopo Charambe Foma na kwamba alikuwa ni mwalimu wa madrasa.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Charambe, John Bazil, alisema kuwa anadhani Said alikuwa na matatizo ya akili.

"Nimehamia hapa juzi juzi, sifahamu sana, lakini taarifa nilizokuwa nazo ni kwamba, Said ana matatizo ya akili ambayo humjia na kuondoka, kitu ambacho watu waliokuwa wakiishi naye walikuwa wanakiona cha kawaida kwa kuwa walimkuta akiwa hivyo," alisema Bazil.


Chanzo: Mwananchi