UNGA WA KILO 201 WADAKWA

Polisi nchini Tanzania wamekamata shehena ya dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 201 katika eneo la bahari kati ya Dar es Salaam na Zanzibar nchini humo.

Kamanda wa kikosi maalum cha kuzuia dawa za kulevya Godfrey Nzowa ameiambia BBC kuwa Watu 12 wanashikiliwa kuhusiana na shehena hiyo.

Kamanda Nzowa amesema dawa hizo za kulevya zimekamatwa na Polisi wa doria baharini muda wa saa sita usiku wa kuamkia Jumanne zikisafirishwa katika Jahazi.

Kwa mujibu wa Kamanda Nzowa Shehena hiyo ilikuwa ikitoka nchini Iran kuelekea nchi au eneo ambalo mpaka sasa bado halijafahamika.

Hivi karibuni kumekuwa na matukio ya kukamata dawa za kulevya aina mbalimbali kupitia viwanja vya ndege,nchi kavu na baharini, ambapo mwaka jana kiasi kikubwa cha dawa za kulevya zilizokamatwa ziliteketezwa