20 WAJERUHIWA KATIKA GHASIA BUKAVU

Watu ishirini wamejeruhiwa baada ya polisi kufyatua risasi katika mji wa Bukavu, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

Ghasia zilitokea pale polisi ilipojaribu kumzuia kiongozi wa upinzani asihutubie wafuasi wake.

Vital Kamerhe ambaye alikuwa hapo zamani spika wa Bunge na pia msaidizi wa karibu wa Rais Joseph kabila, aliyejiunga na upinzani miezi michache kabla yauchaguzi wa mwaka 2011, anafanya ziara ya amani mashariki mwa Congo, eneo lililoathirika na vita vya karibu miaka 20.

Kamerhe alisema kuwa polisi waliwapiga risasi wafuasi wake wakati wa mkutano wao mjini Bukavu.

Gavana wa jimbo alikanusha madai kuwa watu walipigwa risasihuku akisema kuwa wafuasi ndio walikuwa wakali kwa polisi.

Ifikapo mwaka 2016, wakati uchaguzi mkuu utakapofanyika, Kabila atakuwa amekamilisha mihula miwili mamlakani na anazuiwa na katiba kugombea tena urais Makundi kadhaa ya upinzani yanamtuhumu Kabila kwa kutaka kubadilisha katiba na kutaka kugombea muhula wa tatu.

Kamerhe aliyekuwa mmoja wa watu wakuu katika kampeini ya uchaguzi wa Urais wa Kabila mwaka 2006 alisema kuwa Kabila anaogopa upinzani kujitokeza dhidi yake kwa sababu hana ushawishi mkubwa sana.

Alivunja uhusiano wake na Rais Kabila mwaka 2010 baada ya Kabila kuruhusu majeshi ya Rwanda kuingia nchini humo kuwasaka wapiganaji wa kihutu Mashariki mwa Congo.

Alibuni chama chake cha kisiasa na kushindana na Kabila mwaka 2011 huku akishikilia nafasi ya tatu.

Kamerhe alisema kuwa maafisa wakuu walimruhusu kufanya mkutano wake katika uwanja wa michezo wa Bukavu lakini kumbe uwanja huo ulikuwa umepangiwa kutumiwa kwa mechi.