SABATO MATENGENEZO LAPIGWA MARUFUKU

Serikali wilayani Kakonko mkoani Kigoma, imelipiga marufuku kanisa moja la dini ya Kikristo linaloitwa Sabato Matengenezo, ambalo limeanzishwa na watu sita ambao kwa sasa wanashikiliwa polisi.

Waumini hao wanadaiwa kuwanyima haki za msingi watoto wao, ikiwamo kuwakataza kwenda shule, kupata matibabu katika hospitali na zahanati kwa kile wanachodai kuwa imani ya dini yao hairuhusu.

Habari kutoka kijijini hapo, zinasema kutokana na tukio hilo, watoto wawili wamefariki dunia baada ya wazazi wao kuacha kuwapeleka hospitali kwa kile walichodai kuwa ni kimyume na imani ya dini yao.Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Kigoma, Dismas Kisufi alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo pamoja na vifo hivyo alisema hajapata taarifa ya tukio hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Peter Toyima naye alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alikiri kuwa na taarifa kuhusu kanisa hilo na kusema kanisa hilo jipya limekuja na sera ya kuwazuia watoto wao kwenda shule, hospitali kupata matibabu nakulipa nauli wanapokuwa katika vyombo vya usafiri, hatua inayopingana na azma ya Serikali kutaka watoto wapate haki zao za msingi.

"Serikali haitakuwa tayari kuona baadhi ya watu wanazuia haki za msingi za watoto wao kwa kuwakataza kwenda shule, kupata matibabu katika hospitali au zahanati kwa kisingizio cha imani zakidini, jambo hili haliwezi kukubalika," alisema Toyima.

Waumini hao wanaoshikiliwa na polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi Kakonko wametajwa kuwa ni; Ndayizeye Gervas, Majaliwa Gervas, Paschal Silvanus, Inocent Ernest, Medadi Laurent na Julietha Medadi ambao ni wakazi wa Kijiji cha Nyabibuye, Kata ya Rumashi wilayani Kakonko na wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mkuu huyo wa wilaya, aliwataka wananchi kuachana na dini zisizoeleweka na zinazoleta mifarakano katika jamii, na wakati wengine wakisisitiza kuwapatia elimu watoto wao, kanisa hilo linakataza kusomesha watoto kwa madai kwamba kuwapeleka shule na hospitali ni dhambi kwa Mungu.

Alisema jitihada za Serikali wilayani Kakonko zimesaidia kuwachukua watoto wawili waliofaulu kwenda Sekondari za Kanyonza na Nyamtukuza na kuwawezesha kuanza masomo ya kidato cha kwanza.

Kanisa hilo jipya linadaiwa kujimega kutoka katika Kanisa la Sabato ambalo ni moja wapo ya makanisa yenye idadi ndogo ya waumini mkoani Kigoma ikilinganishwa na Kanisa Katoliki, Anglikana na Assemblies of God.