MCHUNGAJI MTIKILA ASISITIZA KWENDA MAHAKAMANI KUDAI TANGANYIKA HURU

*Asisitiza kwenda Mahakamani wiki ijayo, kudai Tanganyika huru LICHA ya kuteuliwa kuwa mmoja wa wajumbe wanaounda Bunge la Katiba, Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameibuka na kubeza uteuzi huo, akidai kuwa kibarua hicho ni sawa na kufanya kazi kama roboti kwa manufaa ya utawala na si ya wananchi.

Kauli ya Mchungaji Mtikila imekuja ikiwa ni siku mbili tu tangu Ikulu itangaze majina ya wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba, linalotarajiwa kuanza vikao vyake Februari 18, mwaka huu, mjini Dodoma.


Akizungumza kwa nyakati tofauti, Mchungaji Mtikila alisema kuteuliwa kwake hakumzuii kudai madai yake ya siku nyingi kuhusu serikali ya Tanganyika na kwamba suluhu anayoiona sasa ni kuundwa kwa serikali ya mpito.

"Hii ni roboti inayokwenda kufanyakazi ya wenye utawala, si kwa manufaa ya wananchi, azima yanguya kwenda mahakamani iko pale pale, kuchaguliwa kwangu hakuizimi, lazima iundwe serikali ya mpito ili tumpate mama yetu Tanganyika," alisisitiza Mchungaji Mtikila.

"Kuteuliwa kuingia katika Bunge la Katiba hakubadilishi mtazamo wangu kwa Watanganyika, huwezi kutafuta hatma ya Watanzania wakati kuna Watanganyika haki zao zinakandamizwa, hili litakuwa Bunge la wendawazimu, kwanza mchakato mzima wa kudai Katiba mpya haukuwa halali, hivyo unatakiwa ushughulikiwe," alisema Mchungaji Mtikila.

Mchungaji Mtikila, ambaye amekuwa na msimamo wa kudai Serikali ya Tanganyika kwa miongo na miongo, alisema mara atakapofika kwenye Bunge hilo katika kikao cha kwanza, atatoa hoja ya kutaka iundwe kwanza Katiba ya Watanganyika na endapo hatosikilizwa, itampa urahisi wa kufungua kesi ya kudai Tanganyika huru.

"Wakikataa hoja hiyo, ina maana dhamira yangu ya kufungua kesi iko pale pale na kesi yenyewe nitaifungua mapema wiki ijayo. Nikishaifungua kesi ina maana mchakato mzima wa Bunge la Katiba utasimama."

Ikumbukwe kuwa tunapozungumzia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wenzetu Wazanzibari wao walishajitoa siku nyingi, kwasababu wamefuta kile kipengele cha wao kuwa nchi ndani ya Muungano.

Kwamba wao ni nchi inayojitegemea, nafasi hii niliyoipata nitakwenda kuitumia kutibu wagonjwa, kwasababu ninayo ya kuzungumza. Uteuzi huu umeongeza mafuta katika moto nitakaouwasha juu ya Watanganyika kupata Katiba yao," alisema Mchungaji Mtikila.

Alisema kitendo cha uhuru wa Tanganyika kubatilishwa na kuungana na Wazanzibari hakikubaliki na kinakwenda kinyume na matakwa ya wananchi.

Akisisitiza kuhusu hilo, alisema uhuru ni haki kuu ya watu wote duniani, ambayo ilisababisha kuundwa kwa Umoja wa Mataifa mwaka 1945 (The right to self determination).


Kutokana na hilo, Mtikila alisisitiza kuwa uhuru wa Watanganyika ni haki ya Watanganyika wenyewe, hivyo wana wajibu wa kuutunza uhai wao katika mipaka ya ardhi kwa utaratibu waliojiwekea kwa kutumia maziwa na asali yao.

Mtikila alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa katika kesi ya madai ya Tanganyika huru, mmoja wa washitakiwa atakuwa ni hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere, kutokana na kuhusika katika kuwapunguzia Watanganyika ubinadamu kwa kulazimishwa kuwa 'watumwa wa Wazanzibari'.


"Tunataka Mahakama ya Kimataifa itupatie haki ya uhuru wetu (The right to self determination of the people of the Republic of Tanganyika) kama binadamu wengine wote katika mipaka ya nchi zao, tunaiambia mahakama yaulimwengu kwamba muungano ni kongwa la utumwa katika Tanganyika," alisema Mchungaji Mtikila.

Mchungaji Mtikila, ambaye ni miongoni mwa wanasiasa waanzilishi wa siasa za mageuzi, mara kadhaa amekuwa akiushambulia utawala wa CCM tangu enzi za hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mpaka sasa chini ya Rais Jakaya Kikwete, anatazamwa kuleta changamoto kubwa ndani ya Bunge hilo, kutokana na hoja yake ya kudai Tanganyika huru.

Mwanasiasa huyo alianza kudai serikali huru ya Tanganyika tangu enzi za utawala wa Hayati MwalimuNyerere, hiyo ikiwa kabla ya kuundwa kwa kundi la wabunge 55, maarufu kama (G55), ambalo lilikuwa na mtazamo kama huo.

Hoja ya kurudisha serikali ya Tanganyika ambayo ilianza kutikisa tangu miaka ya nyuma, inatarajia kujirudia safari hii katika Bunge la Katiba, kutokana na baadhi ya wajumbe kupishana katika maoni yao, hususani kwenye vyama.

Hatua hiyo inatokana na sehemu kubwa ya wabunge na wafuasi wa CCM kutaka muundo wa serikali mbili, huku upande mwingine ukiungana na mapendekezo ya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba mpya, Jaji Joseph Warioba.

Wengi wanamtazama Mtikila katika kundi linalotaka mfumo wa serikalitatu, lakini mwenye hoja tofauti yakudai kwanza Tanganyika huru, kabla ya mchakato wa kuunda Katiba ya Muungano, jambo ambalo linaweza kuliweka Bunge njia panda, endapo ataamua kung'ang'ania msimamo wake huo.