GAVANA AANZISHA USHURU WA KUAGA MAITI

Katiba Mpya ya Kenya imeanzisha mambo mengi mapya. Imeshusha madaraka kwa wananchi na kuwapa madaraka makubwa magavana ya kuamua mambo mbalimbali.

Kenya ilizindua Katiba mpya Agosti 27 mwaka 2010 kwenye sherehe iliyojaa mbwembwe katika bustani ya Uhuru, Nairobi.

Hiyo ilikuwa baada ya Wakenya kupiga kura kwa wingi wakiunga mkono Katiba Mpya. Badala yake katiba imekuwa chungu kwa Wakenya kwa magavana kuaanzisha ushuru wa aina mbalimbali ikiwemo ushuru wa kuaga maiti.

Inatafsiriwa kuwa, magavana wametumia mamlaka yao kunyanyasa wananchi katika kaunti.

Katika Kaunti ya Kiambu, inayoongozwa na Gavana William Kabogo, kuna ushuru mpya unaotozwa kwa familia iliyopoteza mpendwa ama wapendwa wao.

Hakuna anayekubaliwa kumzika mfu wao bila kulipa ushuru huo. Pia, huwezi kuchinja mfugo wako nyumbani bila kulipa ushuru!
Katika Kaunti ya Kakamega, Gavana amebuni ushuru wa kuku ambapo kila mfugaji atalipa Sh20 kwa kila kuku anayemfuga.


Pia, watu wanapoomboleza, lazima walipe ushuru wa kuomboleza haswa wanapotazama mwili wa marehemu.
Ukiutazama zaidi ya mara mbili, utalipa ushuru zaidi ya mara moja!
Watu hawajui la kufanya na wana majuto makuu kwa kukaribisha Katiba mpya 2010. Walipokuwa wanaipitisha walikuwa na matumaini kwamba ingebadilisha maisha yao kwa kuleta utawala na huduma za Serikali Kuu karibu yao.

Wakati huo wa mchakato wa Katiba mpya, Makamu wa Rais William Ruto alikuwa katika upande uliokuwa ukipinga Katiba hiyo.

Hata hivyo, Muungano wa Jubilee ulipochukua hatamu ya uongozi, Ruto na Uhuru Kenyatta waliapa kuilinda na kuitetea Katiba hiyo.

Katiba ikawa mwanzo wa Serikali mpya iliyoshusha zaidi madaraka kwa wananchi hadi ngazi ya Kunti, kwa lugha ya Kenya inaitwa Serikali ya Ugatuzi, ambapo mipaka ya nchi iliyowekwa wakati wa ukoloni, iligawanywa upya ili mipaka mipya ya Kaunti 47 iundwe.

Machi 4 mwaka 2013, uchaguzi mkuu ukafanyika na viongozi mbalimbali wakiwamo magavana wakachaguliwa, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Kenya kuwa na viongozi wa aina hii.

Sasa Kenya ina magavana 47, baadhi ya watu wanaona kuwa viongozi hawa wanakuwa kama miungu watu ambao Wakenya hawana budi kumshukuru Mola kwa sababu yao.


Hali hiyo inatokana na tuhuma za ufisadi zinazowakabili baadhi magavana, hali iliyowakasirisha Wakenya walio wengi.

Mmoja wa anayekabiliwa na tuhuma hizi ni Martin Wambora wa Kaunti ya Embu. Kiongozi huyu alipoteza wadhifa wake wiki iliyopita, baada ya Bunge la Kaunti kupiga kura ya kumwondoa katika wadhifa wa Ugavana.

Wambora alituhumiwa kujihusisha na ufisadi wa hali ya juu, ambapo Kaunti ilipoteza mamilioni ya fedha baada ya zabuni ya kununua mbolea na mbegu za mahindi kwenda mrama.

Mbegu za mahindi hazikumea na mbolea haikuwa nzuri, huo ulikuwa mwanzo wa masahibu ya Wambora yaliyomfikisha mbele ya Kamati ya Seneti iliyosikiliza kesi yake na kuamua kumfuta kazi.


Naibu wake sasa amechukua nafasi yake na kufanya Kenya kupata gavana wa kwanza mwanamke.

Kufutwa kazi kwa Wambora kulifungua mlango wa Bunge la Seneti kuonyesha kati ya seneta na gavana, ni nani mkubwa.

Wakati Seneti ilikuwa ikitoa uamuzi wake kuhusu hatma ya Wambora, maseneta wawili walisema hawatashiriki kwenye zoezi hilo kwa sababu mchakato mzima haukufuata haki.

Seneta mmoja aliyeunga mkono kufutwa kazi kwa Wambora, aliiambia Seneti kuwa, kuanzia sasa magavana watajua'nani kati yao na sisi ndiye ana uwezo wa kumtimua na kumwadhibu'.


Kwa wadadisi wa kisiasa, hatua ya Seneti kumng'oa mamlakani gavana huyo, ni jaribio la maseneta kutoa ujumbe kwa magavana wanaotuhumiwa kuwapuuza viongozi hao haswa katika suala la kupeleka madaraka kwenye kaunti.

Sasa, Wambora ameenda nyumbani kutafuta kingine cha kufanya na Seneti inapanua upeo wake ili inase magavana zaidi wanaoshukiwa kufuja pesa za umma na kubuni sera potofu za kunyonya jasho la wananchi wa kawaida kwa kuwatoza ushuru.

Kusambaza ufisadi
Ufisadi sasa umesambazwa kutoka Serikali Kuu hadi Serikali za Mashinani na kufanya maisha kuingia kwenye mkondo mbaya zaidi.

Fedha zilizopaswa kutumwa kutoka kwenye Serikali Kuu kwenda kwenye kaunti, hazitumiwi ipasavyo.

Badala yake, pesa hizo za maendeleo ya kikaunti zinafujwa na kuelekezwa kwenye miradi bifasi ya magavana na vibaraka wao.

Ajira katika kaunti ni kama sarakasi kwa sababu magavana hawazingatii sheria na kanuni zinazo ongoza uajiri wa wafanyakazi wa umma.

Magavana wanaajiri jamaa zao wasio na ujuzi au elimu na kuwaacha wataalamu waliosomea nafasi husika.


Uchunguzi uliofanywa miezi mitatu iliyopita, unaonyesha kuwa magavana wametenga mamilioni ya fedha kugharimia safari zao za nchi za nje haswa Uingereza, Amerika na Ufaransa.

Seneta inanuia sasa kukata'pembe'za magavana wote na kuna orodha ya majina tisa ya wale wanaotakiwa kufika mbele ya Kamati ya Seneti kujibu maswali kuhusu matumizi ya fedha za umma.

Majibu yatakiwa
Magavana hao tisa wanatakiwa pia kujibu maswali kuhusu ushuru tata walioanzisha katika kaunti zao.

Anayelengwa zaidi ni Gavana wa Kaunti ya Bomet, Isaac Ruto aliyekuwa amezoea kumzomea na kumkosoa Makamu wa Rais kwa hili na lile. Majibizano kati ya hao wawili yalikuwa yakitawala vyombo vya habari.

Gavana Rutto anaonekana kama'mwenye kichwa kikubwa'na anafaa'kurekebishwa'na Seneti ili afuate mkondo unaotakikana.

Lakini Seneti ina haki ya kuwaadhibu magavana wanavyopenda? Nguvu hizi za Seneti kuwaadhibu magavana zimetoka wapi?
Kwa muda mrefu, mashindano katika ya maseneta na magavana kuhusu'ukubwa'yamekuwa yakitawala vyombo vya habari.

Magavana walioandikiwa barua kufika mbele ya Seneti wanasema maseneta wamekosea kisheria kuwataka wafike mbele yao.


Hatua ya kwanza wanayochukua magavana kujaribu kuwazuia maseneta kuwaadhibu ni kutuma maombi ya kesi kwa kwa mahakama ya kisheria ili iamue nani kati yao ni'ndume'ya mwengine.

Mwaka mmoja umeisha tangu Uchaguzi Mkuu umefanyike, lakini kilichodhairi shahiri ni kwamba maendeleo ya kipekee wanayoyazingatia viongozi waliochaguliwa ni kujipiga kifua kuonyesha nani ni mkubwa zaidi ya mwenzake.

Hayo yakiendelea, barabara zimezorota, sekta ya afya imesambaratika na wananchi wamepoteza matumaini, ya kuona siku moja wataishi maisha yanayofaa na kuachana na ufukura wao wa miaka mingi.

Ufisadi umeota mizizi nchini na ni mzigo kwa maisha ya wananchi, hawaoni tofauti kati ya vitendo vya maseneta na magavana.


Hii ni kwa kuwa wengi wao wanashiriki ufisadi. Ni kweli kwamba kama maseneta wangekuwa na nafasi ambayo magavana wanazo, baadhi yao wangefanya kama vile magavana walivyofanya kwa kufuja mali za umma na kuendeleza ukabila.

Katiba Mpya ilikuwa inaonekana kama baraka kwa Wakenya, lakini kwa hakika imeleta shida nyingi na kufanya maisha kuwa magumu zaidi.

Wanaoumia ni wananchi wa kawaida, huku viongozi wakiendelea kujilimbikizia mali bila kutoa jasho.

Wanaendelea kutajirika huku wananchi wakihangaishwa na maisha. Mwokozi wao ni nani?


Chanzo: Mwananchi